SCHOLES ANOGEWA OLD TRAFFORD


KIUNGO  wa Manchester United, Paul Scholes yuko tayari kurefusha kwa msimu mmoja, awamu ya pili ya uchezaji wake klabuni Old Trafford.
Nyota huyo mkongwe, alirejea dimbani Januari mwaka huu ikiwa ni  miezi kadhaa baada ya kustaafu soka, akifuata  ombi la kocha wa United Sir Alex Ferguson aliyekuwa ameelemewa na idadiya majeruhi zaidi kwenye idara ya kiungo.
Kurejea kwake imekuwa msaada mkubwa kwa United kwani kumeiwezesha kuwashusha mahasimu wao wa  Man City katika kilele cha Ligi Kuu ambayo ilikalia mwezi Oktoba mwaka jana.
Kwa sasa Scholes anataka kufuata nyayo za mkongwe mwenzake Ryan Giggs (38) kiasi cha kuhitaji msimu mwingine wa kupigania heshima ya klabu hiyo aliyopata nayo mafanikio yaliyotukuka.
Scholes amekuwa sehemu muhimu ya kikosi cha United katika jumla ya mechi 15, kuanzia pale alipoingia akitokea benchi na kuisaidia klabu yake kuichapa City mabao 3-2 katika mechi ya Kombe la FA iliyopigwa Januari 8.
Scholea  ameanza kikosi cha kwanza mara nane kati ya mechi hizo, akifunga mabao mawili na kuthibitisha aina ya uimara alionao. Kocha wake Ferguson amemzungumzia akisema: "Kiwango chake kimekuwa ni cha kuvutia mno."
Scholes alistaafu soka mwishoni mwa msimu uliopita, lakini ghafla akalalamika kutojisikia vema kuukosa mchezo aupendao, wakati huo akibeba jukumu la kukinoa kikosi cha nyota wa akiba wa United kwenye uwanja wa Carrington.

Comments