RUVU SHOOTING YAIBAMIZA MTIBWA SUGAR 3-1


Na Victor Masangu, Pwani

MAAFANDE wa Ruvu Shooting ya Pwani, jana waliutumia vema uwanja wao wa nyumbani wa Ruvu Mabatini mjini hapa, baada ya kuwachapa ‘Wakata Miwa wa Manungu’ Mtibwa Sugar ya Morogoro kwa mabao 3-1.
Bao la kwanza la Ruvu lilifungwa na mshambuliaji Hassan Dilunga kunako dakika ya 39, kabla ya Mohammed Kijuso kufunga la pili dakika ya 44. Hadi mwamuzi Judith Gamba kutoka Arusha anapuliza kipenga cha mapumziko, Ruvu ilikuwa mbele kwa mabao 2-0.
Kipindi cha pili kilianza kwa moto ule na kwa mara ya pili, Dilunga akaifungia Ruvu bao la tatu na la mwisho kunako dakika ya 49. Bao la kufutia machozi kwa Mtibwa lilifungwa na Thomas Mankana.
Katika mechi hiyo, Paul Ngalemwa wa Ruvu alitolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 76 na mwamuzi Gamba, baada ya kufanya uzembe wa kuchelewesha mpira, kupunguza kasi ya ‘Wana-Tam tam’.
Hadi filimbi ya mwisho ya mwamuzi, Ruvu Shooting iliibuka na ushindi huo wa mabao 3-1, ambapo Kocha wa maafande hao Charles Boniface Mkwasa, aliwapongeza vijana wake na kusema nguvu zao wanazielekeza katika mechi ijayo dhidi ya Simba.
“Nawapongeza sana vijana wangu kwa aina ya upiganaji waliouonesha dimbani na kuibuka na ushindi huu. Nguvu zetu sasa tunazielekeza kwa Simba, tukiamini kwamba tukicheza vema kama leo tutapata matokeo mazuri,” alisema Mkwasa. 
Kwenye Uwanja wa Chamazi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, Villa Squad iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Moro United, huku mabao ya Villa yakiwekwa kimiani na Nsa Job Mahenya dakika ya 23 na Omari Issa ‘Berbatov’ dakika ya 90.
Bao la Moro United lilifungwa na Rajabu Zahir dakika ya 44.

Comments