RONALDO AZIDI KUCHAFUKA MABAO LA LIGA


MRENO Cristiano Ronaldo amefikisha mabao 30 msimu baada ya kuwawezesha vinara wa La Liga, Real Madrid kuibuka na ushindi wa 5-0 Jumapili dhidi ya Espanyol kwenye Uwanja wa Bernabeu na kuendelea kusimama kileleni kwa pointi 10 zaidi dhidi ya mabingwa watetezi, Barcelona.
Mshindi huyo wa tuzo ya Kiatu cha Dhahabu Ulaya kwa mabao yake 40 msimu uliopita, alifunga bao la kwanza akimalizia kazi nzuri ya Gonzalo Higuain dakika ya 23 na kufikisha mabao 38 katika mashindano yote msimu huu.
Sami Khedira alipiga la pili baada ya gonga safi kati yake na Mjerumani Mesut Ozil dakika ya 38 na Higuain akapiga la tatu dakika tatu tangu kuanza kipindi cha pili.
Kaka alitengeneza la tatu, akafunga la nne dakika ya 66 na akatengeneza pia bao la tano lililotiwa kimiani na Higuain dakika ya 78.
Timu ya Jose Mourinho sasa imekaribia kabisa kutwaa taji la kwanza ndani ya miaka mine la La Liga, baada ya kufikisha pointi 67 wakiwa wamebakiza mechi 13.
Mabingwa Barcelona walimpoteza Gerard Pique dakika ya 46 baada ya kupewa kadi nyekundu, lakini bado tu wakaifunga Sporting Gijon mabao 3-1 nyumbani na kufikisha pointi 57 Jumamosi.

Comments