NAFASI NYINGINE KWA BARCA KUIKARIBIA REAL LEO

LEO Barcelona inaweza kupunguza pengo la pointi inazozidiwa na Real Madrid katika La Liga na kubaki pointi tano, iwapo watashinda mechi dhidi ya wageni wao, Granada.
Hiyo inafuatia Real kulazimishwa sare ya 1-1 nyumbani na Malaga juzi.
Kikosi cha Jose Mourinho kilinyimwa ushindi wa 12 mfululizo kwa bao la dakika ya mwisho la Santi Cazorla, hivyo kufufua matumaini ya Barca kutwaa taji la nne mfululizo la La Liga.
Real, ikiwa na pointi 71 dhidi ya 63 za Barca, zikiwa zimebaki mechi 11, wanakabiliwa na mechi ngumu ugenini kesho dhidi ya Villarreal, ambao wanapigana kurejea matawi ya juu.
Utakuwa ni mtihani mgumu kwa Miguel Angel Lotina, kocha wa tatu Villarreal msimu huu, aliyetambulishwa jana baada ya kufukuzwa kwa Jose Molina.
"Kwangu inaonekana sare ni sehemu ya mchezo," alisema Mourinho baada ya mechi na Malaga.
"Sote tunafahamu kuna mechi 11 zimebaki na pointi 33 mbele, ambayo inamaanisha mbio za ubingwa bado zipo wazi," alisema Mreno huyo.

Comments