MWAMUZI ADUNDWA ZANZIBAR


  CHAMA cha soka Zanzibar (ZFA), kimeishusha madaraja mawili, kuwafungia mwaka mmoja viongozi wote na wachezaji saba wa timu ya Ngome FC baada ya juzi kumpiga mwamuzi msaidizi Mohammed Ibrahim, baada ya kumalizika kwa mechi ya Ligi daraja la kwanza, ambayo walifungwa mabao 2-1 na Bandari iliyopigwa kwenye uwanja wa Fuoni.
Tukio hilo linakuja baada ya hivi karibuni wachezaji wa Kikwajuni kumshushia kipigo cha aina yake, mwamuzi Waziri Sheha.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu kutoka Zanzibar jmchana Msemaji wa ZFA, Munir Zakaria, alisema kuwa uamuzi huo umetolewa jana baada ya kikao cha kamati tendaji ya ZFA iliyoketi kujadili kitendo hicho kilichotokea juzi.
Alisema baada ya kupitia ripoti ya mwamuzi na ile ya kamisaa na kuwasikiliza wahusika, ZAFA iliamua kutumia kanuni ya 25 inayozungumzia adhabu zinazostahili kutolewa kwa wanaowapiga waamuzi na ikizingatiwa kuwa vitendo hivyo vinataka kukithiri katika soka la Zanzibar.
“Baada ya kuona vitendo vya kuwapiga waamuzi vinakithiri katika viwanja vya soka Zanzibar kamati tendaji ya ZFA iliyoketi leo asubuhi ‘jana’ imeamua kuishusha kwa madaraja mawili kwa mujibu wa kifungu cha sheria ibara ya 25, imewafungia viongozi wake wote mwaka mmoja, pamoja na wachezaji pia wote watatakiwa kulipa faini ya sh 100,000 kila mmoja,” alisema Zakaria.
Aliwataja wachezaji waliofungiwa kwa mwaka mmoja na kutozwa faini ya sh 100,000 kuwa ni Njema Francis, Khatibu Hussein, Idi Kambi, Khalid Shaame, Ahmed Omari, Hassan Ramadhani na Abdallah Omari, ambao ndio waliobainika kuwa.
Zakaria aliwaonya viongozi wa klabu, wachezaji na mashabiki kuacha tabia ya kuwapiga waamuzi badala yake akawataka kukata rufaa au kuwasilisha mamalalamiko yao kwa maandishi iwapo wana malalamiko dhidi ya waamuzi na ZFA itayafanyia kazi mara moja.


Comments