MUSSO AUNGA MKONO KIFUNGO CHA KINA TEGETE


KOCHA Msaidizi wa timu ya Moro United ‘Watoto wa Tabata’ Yusuph Macho ‘Muso’, amesema vurugu zilizofanywa na wachezaji wa klabu kongwe ya Yanga katika mchezo wao dhidi ya Azam Fc zinapaswa kulaaniwa na kila mpenda michezo nchini.
Macho, nyota wa zamani wa Simba na Yanga, aliyasema hayo jijini Dar es Salaam jana, wakati akizungumza na Tanzania Daima kwa njia ya simu, kuhusiana na vurugu zilizoanza kujitokeza katika ligi kuu ya soka Tanzania bara.
Alisema, kinachomsikitisha ni kuona, vurugu hizo zinafanywa na wachezaji wa timu zinazoitwa kongwe hapa nchini, jambo linalotoa picha mbaya kwa timu nyingine na kwa vijana wanaochipukia katika ulimwengu wa soka.
“Ni muhimu hasa kwa hawa wachezaji wa timu kubwa na wenye majina makubwa, kuzuia mihemko yao kwa kuwa jamii inawaangalia wao kama mifano ya mambo mazuri, sasa wanapofanya vitu visivyoeleweka ni kudhalilisha fani ya soka nchini,” alisema Muso.
Aliongeza kuwa, wachezaji waliodhibiwa wasipoteze muda wao kumtafuta mchawi, bali wakae na kutuliza akili kwa ajili ya kuhakikisha hawarudii makosa kama hayo, kila watakapopata fursa ya kuingia uwanjani.

Comments