MOURINHO KUREJEA CHELSEA


BILIONEA Roman Abramovich anaweza kumuangukia Jose Mourinho, baada ya kocha huyo wa zamani wa Chelsea, kupendekezwa kwa kiasi kikubwa kurejea Stamford Bridge msimu ujao kupiga tena kazi, kufuatia kutimuliwa kwa Andre Villas-Boas.
Abramovich amemwaga Villas-Boas Jumapili zikiwa ni saa 24 baada ya kipigo cha 1-0 kutoka kwa West Bromwich Albion, kinachowaangushia The Blues nafasi ya tano katika Ligi Kuu.
Kiungo wa zamani wa Chelsea, Roberto Di Matteo, ambaye alikuwa akifanya kazi msaidizi wa Villas-Boas, amepewa ukocha wa muda hadi mwsiho wa msimu.
Mtihani wa kwanza wa Di Matteo ni mechi ya marudiano ya Raundi ya Tano Kombe la FA dhidi ya timu ya Daraja la Kwanza, Birmingham kwenye Uwanja wa St Andrews kesho.
Baada ya hapo, Mtaliano huyo atakuwa na kibarua cha kuirudisha Chelsea kwenye Top Four, inayowahakikishia kucheza Ligi ya Mabingwa msimu ujao na pia atakuwa na kibarua cha kuupiku ushindi wa 3-1 walioupata Napoli katika mechi ya kwanza ya hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa.
Lakini habari rasmi ni kwamba, Abramovich sasa anasaka kocha wa nane katika miaka nane ya kuimiliki klabu hiyo ya Magharibi mwa London.
Tangu ainunue Chelsea mwaka 2003, Abramovich amewafukuza Claudio Ranieri, Mourinho, Avram Grant, Luiz Felipe Scolari, Carlo Ancelotti na sasa Villas-Boas.
Kocha wa Real Madrid, Mourinho ameiwezesha timu hiyo kuongoza Ligi Kuu ya Hispania, La Liga licha ya ushindani mkubwa kutoka kwa Barcelona.
Tayari Mourinho anahisi hapendwi Hispania, kutokana na misukosuko  na uhusiano mbaya uliojengeka kati yake na wadau wa timu hiyo na vyombo vya habari.
Bado anawasiliana kwa sms na watu wazito ndani ya Chelsea nab ado anapendwa sana Stamford Bridge na wachezaji na mashabiki.
Kudhihirisha tetesi hizo, Mourinho alionekana London wiki iliyopita akinunua nyumba mpya.
Watu wa karibu na Mreno huyo wanasema yuko tayari kurejea England na inaelezwa hivi sasa yupo kwenye mawasiliano mazuri na Abramovich baada ya kuondoka Chelsea, Septemba mwaka 2007.
Kocha wa zamani wa Liverpool, Rafael Benitez, ambaye kwa sasa hana kazi baada ya kutupiwa virago Inter Milan, naye anatajwa kuwa kocha mpya wa Chelsea.
Wengine ni kocha wa Barcelona, Pep Guardiola, ambaye amebakiza mkataba wa mwaka mmoja na mabingwa wa Hispania na labda yu tayari kwa changamoto mpya baada ya mafanikio makubwa Nou Camp.

Comments