MOURINHO HANA AMANI KWA CSKA


KOCHA Jose Mourinho amepuuza madai kwamba anaweza kujiuzulu ukocha Real Madrid, iwapo timu hiyo haitafuzu Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mbele ya CSKA Moscow ya Urusi.
Mchezo huo umekaa vibaya kufuatia matokeo ya sare ya 1-1 mjini Moscow, ingawa Real inapewa nafasi kubwa ya kusonga mbele katika mchezo wa marudiano kesho kwenye Uwanja wa nyumbani, Santiago Bernabeu.
Mourinho amesema kwamba anahofia desturi ya mchezo kutobarika kuliko mustakabali wa kazi yake iwapo akifungwa.
"Mustakabali wangu hauwezi kuamuliwa na matokeo ya Jumatano, labda itokee klabu inifukuze tukishindwa kufuzu,"alisema Mreno huyo, ambaye klabu yake inaongoza Ligi Kuu Hispania ikiwazidi pointi 10, wapinzani wao na mabingwa watetezi, Barcelona.
"Lakini pointi yangu ya msingi ni kwamba, matokeo hayatabdili kitu. Mchezo wa kwanza ulikuwa na mkangayiko ambao unaacha nafasi wazi. Kuelekea kesho ninauhofia sana mchezo, ambao unaweza kutoa matokeo yoyote ya kustaajabisha."
Mourinho pia anaamini kupiga kwake kazi Chelsea na Inter Milan –aliowapa taji la Ligi ya Mabingwa na baadaye Bernabeu mwaka 2010 – itakuwa faida kwake kuelekea mchezo huo.
"Naifahamu CSKA tangu nikiwa Chelsea na Inter na ninafahamu ni timu inayokanganya kucheza nayo. Wanakufuata kwa kasi, wana mashambulizi makali ya kushitukiza na wana safu ngumu ya ulinzi. Lakini nafikiri tuna spana za kuwapiku."
Mourinho alipoulizwa kuhusu washambuliaji wake, Gonzalo Higuain aliyerudi kwenye fomu na Karim Benzema aliyekuwa majeruhi, alisema; "Nilikuwa nina matatizo wakati Higuain hakuwa kwenye fomu au Benzema alipokuwa majeruhi. Kwa sasa, tatizo hilo halipo tena," alisema Mourinho. "Kwa ujumla, kuwa nao wote ni jambo zuri linalowezekana."

Comments