MIKOA YAHADHARISHWA KUTUMIA WACHEZAJI VIJEBA COPA COCA COLA

Mkurugenzi wa Ufundi na Afisa Maendeleo wa Shirikisho la Soka(TFF) Sunday Kayuni,akizungumza wakati ufunguzi wa semina elekezi ya msimu wa mashindano ya Copa Coca Cola 2012 kwa Makatibu wa vyama vya Mikoa jijini Dar es Salaam jana 


WADHAMINI wa Mashindano ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17, maarufu  Copa Coca Cola wanaratajia kutumia Sh zaidi ya bilioni mbili katika msimu wa mwaka huu. 
Mkurugenzi wa Mahusiano wa Kampuni ya vinywaji Baridi Coca Cola, Tanzania, Evance Mlelwa alisema kila mwaka, wamekuwa wakiboresha udhamini wa mashindano hayo. 
Mlelwa alisema hayo, wakati wa semina elekezi ya makatibu wa vyama vya soka vya mikoa  nchini, iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 
Alisema msimu uliopita kampuni hiyo ilitumia Sh bilioni 1.5 kwa ajili ya uendeshaji wa mashindano hayo. 
Mlelwa alisema kamapuni hiyo inaingia mwaka wa sita kudhamini mashindano hayo, ambayo yamekuwa na mafanikio makubwa. 
Kwa upande wa Makamu wa Kwanza wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Athuman Nyamlai alisema kumekuwemo na changamoto kubwa katika mashindano hayo. 
Nyamlani alisema moja ya changamoto hiyo ni gharamu kubwa ya uendeshaji wa mashindano hayo, ambapo viongozi wengi wa mikoa wamekuwa wakilalamikia udhamini ni mdogo. 
Alisema pamoja na malalamiko hayo, wadhamini hao wamekuwa wakiongeza udhamini wao kila mwaka ili kukidhi matakwa ya mashindano hayo. 
Nyamlani alisema kwa miaka sita ambayo wamekuwa wakishirikiana na Coca Cola kumekuwa na mafanikio makubwa katika kuendeleza soka hususan vijana. 
Alisema kwa suala la kugushi umri wa wachezaji limepungua kwa asilimia 95,  baada ya baadhi ya viongozi kufungiwa kujihusisha na soka. 
Nyamlani alisema tatizo la kudanganya umri si la Tanzania pekee bali ni la dunia nzima, lakini wataendelea kulikemea ili waweze kujenga timu bora ya vijana itakayokuwa na mwelekeo wa 
mbele. 
Naye, Mkurugenzi wa Idara ya Michezo nchini, Leonald Thadeo alisema mashindano hayo, yamekuwa na umuhimu mkubwa katika kuendeleza soka .
Thadeo aliwataka viongozi wa makatibu wa mikoa kuwa na ubunifu wa kuandaa mashindano mbalimbali ambayo yanaleta wadau pamoja. 
Hata hivyo, aliwaomba wadhamini wa mashindano hayo kuona umuhimu wa kushirikiana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), katika kuhakikisha wanawaendeleza wachezaji wanaochaguliwa kuunda timu ya Taifa. 
Mashindano hayo yanatarajia kuanza Machi 31 mwaka huu, ngazi ya wilaya.

Comments