MANCINI ATAKA WACHEZAJI WAPIMWE ZAIDI

KOCHA wa Manchester City Roberto Mancini amesema wachezaji wa Ligi Kuu hawana budi wapimwe afya zao mara mbili kwa mwaka.
Mancini anahisi utaratibu wa upimaji wa sasa "hauna uhakika" sana.
"Wakati nilipoangalia utaratibu wetu wa matibabu miaka miwili iliyopita, niliingiwa na hofu. Nilisema tunahitaji kufanya zaidi ya hapa," alisema.
Mancini ametoa maoni yake baada ya Mtendaji Mkuu wa Ligi Kuu Richard Scudamore kusema kutakuwa na utaratibu wa kupitia masuala ya upimaji baada ya Fabrice Muamba kuanguka na kuzirai kutokana na matatizo ya moyo.
Watu wa huduma ya kwanza walitumia dakika sita wakijaribu kuamsha mapigo yake ya moyo baada ya kiungo huyo wa Bolton kupoteza fahamu walipocheza na Tottenham Hotspur siku ya Jumamosi.
Kiwango cha uangalizi alichopatiwa kimesaidiwa sana kutokana na mabadiliko yaliyowekwa na Ligi Kuu baada ya mlinda mlango wa Chelsea Petr Cech kuvunjika fuvu la kichwa mwaka 2006.
Vile vile, meneja wa Manchester City Mancini amesisitiza utaratibu wa matibabu nchini England bado haufanani na wa Italia.
"Tunahitajika kurekebisha na kuneemesha upande wa matibabu kwa wachezaji," aliongeza. "Hali ni bora zaidi Italia.
"Hatuna budi kuwafanyia uchunguzi wachezaji mara kwa mara, pengine mara mbili kwa mwaka na lazima uchunguzi huo uwe sahihi.
"Kilichomtokea Muamba kinaweza kutokea wakati wowote na hilo linawezekana."
Kocha wa Liverpool Kenny Dalglish alisema kwa upande wake anaridhika na kiwango cha muda ambacho wachezaji wanafanyiwa uchunguzi wa afya zao.
"Wachezaji wetu wanachunguzwa afya zao kila baada ya miaka miwili," alisema Dalglish. "Baadhi wanakuja katika klabu kwa uhamisho au kijana wa miaka 17 anafanyiwa uchunguzi mara moja. Sina uhakika wa usahihi wa upimaji huo kwa kila mchezaji.
"Fabrice pia alifanyiwa uchunguzi wa afya yake, nashawishika kuamini mara nne, lakini huwezi kuchunguzwa kila kitu. Huenda bahati haikuwa upande wake."
Muamba alikimbizwa haraka katika chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi wa karibu katika hospitali inayoshughulika kutibu maradhi ya moyo ya London Chest baada ya kupatiwa huduma ya kwanza kufuatia kuanguka na kupoteza fahamu katika dakika ya 42 ya mchezo kuwania Kombe la FA hatua ya robo fainali .
Hii ilikuwa ni hali tofauti wakati Jose Mourinho alipodai kilichomtokea Cech miaka sita iliyopita. Wakati huo akiwa meneja wa Chelsea, alilalamika ilichukua dakika 30 kwa watu wa gari la kubeba wagonjwa kuwasili uwanjani na kumpatia matibabu mlinda mlango wake.
Lakini msemaji wa kituo cha huduma za magari ya kubebea wagonjwa cha South Central Ambulance Service NHS Trust alipinga malalamiko hayo na kueleza iliwachukua dakika saba tu kuwasili.
Hata hivyo Chelsea iliwasilisha malalamiko rasmi yaliyosaidia kufanyiwa marekebisho utaratibu wa Ligi Kuu na wa Chama cha Kandanda.
Kulibuniwa hatua kadha, ikiwemo kuhakikisha gari la kubeba wagonjwa linakuwepo uwanjani kwa ajili ya matumizi ya wachezaji na madaktari wa timu lazima wahudhurie kila mchezo.

Comments