MAN CITY, MAN UNITED SASA MTIFUANO ENGLAND


Kocha wa United Ferguson
WAPINZANI wa Jiji la Manchester, watarejea kwenye mawindo yao ya taji la Ligi Kuu England baada ya kutolewa kwenye michuano ya Ulaya, lakini pia wakionekana kama kuporomoka kiwango.
Baada ya kutolwa kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa, wametolewa pia na kwenye 16 Bora ya Europa League, hivyo wana sehemu moja tu sasa ya kurudishia heshima, kwenye Ligi ya nyumbani, wanapofukuzana kuwania taji.
Vinara wa England, Manchester United walishindwa kufikia ubora wa timu inayoshika nafasi ya saba katika msimamo wa Ligi Kuu Hispania, La Liga, Athletic Bilbao baada ya kutolewa kwa jumla ya mabao 5-3, wakati City waling’olewa na Sporting Lisbon ya Ureno.
"Tunatakiwa kutwaa ubngwa wa Ligi Kuu kuunusuru msimu wetu. Kama hatutatwaa ubingwa wa Ligi Kuu, utakuwa msimu mbaya haswa,"alisema beki wa United, Patrice Evra kuiambia MUTV.
"Sina wasiwasi na Ligi Kuu, kwa sababu wanacheza vizuri na sasa tuko juu, mbele ya Manchester City."
United inawazidi pointi moja jirani zao hao wakiwa na pointi 67 walizovuna kwenye mechi 28 na wanaweza kufikisha pointi nne za kuwazidi wapinzani wao hao Jumapili wakiifunga Wolverhampton Wanderers siku ambayo City hawatakuwa na mechi hadi Jumatano watakapoikaribisha Chelsea.
Kama wataendelea kukamatana hivyo hivyo, basi bingwa ataamuliwa kwenye mechi ya wapinzani wa Manchester, mwezi ujao kwenye Uwanja wa Eastlands.
England imekuwa na mwaka mbaya msimu huu Ulaya, ikiingiza timu moja tu katika Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa, Chelsea, hali inayokuja miaka mitatu baada ya nchi hiyo kuingiza timu tatu kati ya nne kwenye Nusu Fainali.
City angalau wanaweza kujifariji pamoja na matokeo mabaya Ulaya zaidi ya United- kwanza walipangwa kundi gumu katika Ligi ya Mabingwa na kutolewa Europa League  na Sporting hakukuwa kinyela kama kwa jirani zao.
Kocha Roberto Mancini anaamini wachezaji wake watapigana na kutwaa taji la kwanza la Ligi Kuu tangu mwaka 1968.

Comments