MALINZI BOSI KRFA


Jamal Malinzi
JAMAL Malinzi amechaguliwa kwa kishindo kuwa Mwenyekiti mpya wa Chama cha Soka Kagera (KRFA) leo mjini humo, akimbwaga vibaya mpinzani wake, Farid Said kwa kura 22 dhidi ya mbili.
Katibu Mkuu huyo wa zamani wa Yanga, ametangazwa rasmi muda mchahe uliopita mjini Bukoba kwamba ndiye Mwenyekiti mpya wa KRFA, ingawa zoezi la kuhesabu kura za washindi wa nafasi nyingine linaendelea.
Malinzi anakubalika mno kwa sababu wakazi wa Kagera wanaamini ataleta mabadiliko kwa ujumla na kuiinua soka ya mkoa huo ambayo kwa sasa imeshuka.
Akizungumza na bongostaz kwa simu dakika kadhaa zilizopita, mdogo huyo wa Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), alisema anasubiri mambo yakamilike na taratibu zote za kumuidhinisha zikamilike ndipo aeleze mikakati yake ya kuinua soka ya Bukoba.
“Kwa sasa kwa kweli hali ni mbaya kwenye soka yetu kwa ujumla, tunahitaji kuweka mambo sawa kuanzia ngazi za wilaya, hivi mimi nilijitolea kuwania nafasi hii ili kuusaidia mkoa wangu huo,” alisema Malinzi.
Malinzi, ambaye kwenye uchaguzi uliopita wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) alikaribia kumbwaga rais wa sasa wa shirikisho hilo, Leodegar Tenga, tayari kuna tetesi kwamba atawania tena urais wa TFF.

Comments