MAKONGO, LORD BADEN KUCHEZA FAINALI ZA WANAWAKE KESHO


Shule ya Sekondari ya Makongo ya Dar es Salaam na Lord Baden ya Bagamoyo mkoani Pwani ndizo zitakazocheza fainali ya mashindano maalumu ya mpira wa miguu kwa wanawake kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani. 
Fainali hiyo itachezwa kesho (Machi 8 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Karume kuanzia saa 10 kamili jioni. Michuano hiyo ilianza Februari 24 mwaka huu ikishirikisha timu nane za shule za sekondari. 
Michuano hiyo ambayo ni maalumu kwa ajili ya kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani iliandaliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa kushirikiana na Chama cha Mpira wa Miguu cha Wanawake (TWFA). 
Kundi A lilikuwa na shule za Makongo, Goba, Twiga na Lord Baden ambapo zilichezea mechi zake za awali katika uwanja wa Sekondari ya Makongo. Timu zilizounda kundi B na kuchezea mechi zake uwanja wa Shule ya Sekondari Jitegemee ni Benjamin Mkapa, Jitegemee, Kibasila na Tiravi. 
Lengo lingine la mashindano ni kuhamasisha mpira wa miguu kwa wasichana katika ngazi ya shule, kuandaa, kubaini na kuendeleza mafanikio yanayopatikana katika timu ya wanawake ya Taifa. 
Uchaguzi wa timu shiriki ulizingatia mchango wa shule katika kuendeleza mpira wa miguu kwa wasichana/wanawake. Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano hayo ni Zainab Mbiro kutoka Twiga Sekondari.  

Comments