LIGI YA TAIFA KUFANYIKA VITUO VITATU TOFAUTI


Kamati ya Mashindano ya TFF iliyokutana Machi 24 mwaka huu imepitisha michuano ya Ligi ya Taifa Ngazi ya Taifa inayoshirikisha mabingwa wa mikoa ianze Aprili 22 mwaka huu kwenye vituo vitatu tofauti.
 
Wakati Machi 26 mwaka huu ndiyo ilikuwa mwisho kwa vyama vya mikoa kuwasilisha TFF majina ya mabingwa wao, ni mikoa minne tu iliyomudu kufanya hivyo kwa mujibu wa kalenda ya matukio ya TFF.
 
Mikoa hiyo na mabingwa wake kwenye mabano ni Kigoma (Kanembwa FC ya Kibondo), Ruvuma (Mighty Elephant ya Songea), Kilimanjaro (Forest FC ya Siha) na Dodoma (CDA ya Dodoma Mjini).
 
Hivyo Kamati ya Mashindano imeongeza muda hadi Aprili 9 mwaka huu kwa mikoa ambayo haijawasilisha majina ya mabingwa wao iwe imefanya hivyo. Kwa itakayoshindwa ndani ya muda hiyo, mabingwa wao hawatapata fursa ya kucheza ligi hiyo.
 
Kamati imetoa pongezi kwa mikoa hiyo minne kwa kuhakikisha imechezesha ligi yao kwa mujibu wa kalenda ya matukio ya TFF. Pia imepanga makundi matatu ya ligi hiyo. Kundi A lina mikoa ya Rukwa, Mbeya, Ruvuma, Iringa, Morogoro, Lindi na Mtwara.
 
Kundi B lina mabingwa wa mikoa ya Kigoma, Tabora, Shinyanga, Mwanza, Mara, Kagera, Singida na Dodoma. Kundi C ni Dar 1, Dar 2, Dar 3, Pwani, Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara.
 
TFF inakaribisha maombi ya uenyeji kwa kila kundi. Taarifa rasmi itatumwa kwa vyama mikoa kueleza masharti ya kutimiza kabla ya mkoa kupewa kituo cha ligi hiyo.
 
Mshindi katika kila kundi na washindwa bora (best losers) wawili kutoka kwenye makundi yenye timu nane watapanda daraja msimu ujao kucheza Ligi Daraja la Kwanza (FDL).
 
Pia timu zinatakiwa ziwe zimefanya usajili wa wachezaji kufikia Aprili 10 mwaka huu wakati Aprili 11-18 itakuwa ni kipindi cha kutangaza majina na pingamizi.

Comments