KUJITOA STARS KWA BOCCO...TFF YASEMA ANAHITAJI USHAURI NASAHA


MSHAMBULIAJI wa  timu ya soka ya Azam Fc na kinara wa mabao kwenye ligi kuu soka Tanzania Bara, John Raphael  Bocco ‘Adeboyor’ ametangaza kustaafu kuichezea timu ya Taifa ‘Taifa Stars’.
Bocco ambaye ambaye amekuwa mmoja ya wachezaji chaguo la kocha mkuu wa Stars Jan Poulsen,amefikia hatua hiyo kutokana na kuchoshwa na kuzomewa na mashabiki wa soka kila anapopangwa katika kikosi cha Stars na baada ya hatua hiyo sasa atabaki kuelekeza nguvu zake katika timu yake ya Azam.
Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali  za leo, nyota huyo ameshawasilisha barua kwa Shirikisho la soka Tanzania (TFF) juu ya uamuzi wake huo na kuiomba  TFF kulikemea  suala la wachezaji kuzomewa wakiwa na jezi za Taifa kama walivyokemea uharibifu wa  mali za Uwanja wa Taifa.
Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF  Saad Kawemba alisema bado hawajapokea rasmi barua ya BOcco huku akishangazwa na hatua hiyo  na kusema kama ni kweli mchezaji huyo anahitaji ushauri nasaha.
Alisema tatizo linaloonekana ni umri mdogo alionao mchezaji huo ndio unamfanya ajisikie vibaya mashabiki kumzomea hivyo kikubwa kinachohitajika ni viongozi wa TFF pamoja na timu yake ya Azam Fc kukaa naye na kumpa ushauri.
“Hahaha amejiuzulu kuichezea Stars kwa kipi?mimi nadhani umri ndio unamsumbua sasa kwa udogo alionao anastaafu kuichezea Stars hiyo inaleta maana kweli, kimsingi anahitaji ushauri toka wakubwa zake kwani huwezi kuacha kucheza kwa sababu ya kuzomewa na mashabiki kwa umri huo akistaafu Stars ndio inakuwaje?”Alihoji
“Kuzomea ni jambo la kawaida kwa wachezaji, amezomewa Et’oo (Samwel) na kuitwa nyani  au wachezaji wangapi wakubwa duniani wanazomewa na kudhalilishwa kabisa lakini wanapuuza na kuendelea na kinachowahusu,”Aliongeza Kawemba.
Aidha, Kawemba alisema pindi watakapoipata rasmi barua hiyo watakaa na mchezaji huyo na kuongea naye, huku pia wakiangalia ni jinsi gani watatoa elimu kwa mashabiki kuachana na tabia za zomea zomea ambazo zinawavunja moyo wachezaji.

Comments