KOMBE LA UEFA KUKANYAGA BONGO MACHI 26


BIA ya Kimataifa ya Heineken imetangaza udhamini wa ziara ya Kombe la Mabingwa wa Ligi ya Ulaya (UEFA) 2012 katika Afrika Mashariki, ambako litakuwa jijini Dar es Salaam Machi 26 na 27.
Meneja Uhamasishaji wa Heineken, Hans Erik Tuijt, alisema, Heineken, imekuwa na uhusiano na Mabingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, tangu msimu wa 2005/06 na itabakia kuwa moja ya wadhamini wakuu wa ligi hiyo hadi msimu wa 2014/15.
Alisema, ziara hiyo kwa nchi za Afrika Mashariki, itaanzia Nairobi hadi Dar es Salaam kupitia Mombasa na baadaye kurudi Nairobi na kisha kuelekea Shanghai, China, ambako kwa kipindi hicho, wateja watakaonunua bia hiyo, watazawadiwa tiketi ya kwenda kwenye matukio ya kipekee ya kombe hilo na kupata fursa ya kuona uzoefu wa kandanda.
Tuijt alisema; “Kila msimu wa Ligi ya Mabingwa wa Ulaya, Heineken inajitahidi kuwa na mazungumzo na mashabiki. Uzinduzi wa ziara hii ya Kombe la Mabingwa wa Ulaya kwa mwaka huu, unawaletea karibu mashabiki wa mpira wa miguu duniani, kwa tukio ambalo litawawezesha kujumuika na Heineken kwenye mashindano na wakati tunakaribia kwenye fainali, tutashirikiana na mashabiki ili kuonesha uzoefu wa kihistoria,”.
Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa Matukio wa UEFA, David Taylor, alisema, Ligi ya mabingwa UEFA, ina urithi wa muda mrefu na ni nguzo ya soka la klabu za Ulaya. Ziara ya Kombe hili, kimsingi inaelezea ukweli wa jinsi ilivyokubalika duniani na mwitikio uliopo kwa Ligi ya Mabingwa ya Ulaya.

Comments