KLABU LIGI KUU KUPANGA MIKAKATI YA KUIKABILI TFF



VIONGOZI wa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kesho wanatarajiwa kuwa na kikao kizito jijini Dar es Salaam ambacho lengo lake ni  kujadili ‘changa la macho’ walilopigwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Mmoja ya wajumbe wa kamati ya Vilabu vya Ligi Kuu alisema jana kwamba wamefikia kukutana baada ya TFF kuwahadaa kuhusu suala la kampuni ya kusimamia  Ligi Kuu.
Kiongozi huyo alisema kuwa  Kamati ya Ligi Kuu iliyoundwa na TFF haikuwasilisha hoja ya Kampuni katika kikao cha Kamati ya Utendaji kilichofanyika Februari 12, mwaka huu.
Alisema kuwa  mtu ambaye anaingia kwenye Kamati ya Utendaji ya TFF kutoka kwenye Kamati yao ni Mwenyekiti wao pekee, Wallace Karia.
“Karia pekee ndiye Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF ambaye kutoka kwenye Kamati ya Ligi Kuu iliyoundwa na TFF anaingia kwenye kikao cha Kamati ya Utendaji.
Lakini ajabu, habari ambazo tumezipata ni kwamba hajawasilisha hoja hiyo na hakuna mtu aliyeinuka kuhoji kuhusu suala la kampuni,” alisema kiongozi huyo. 
Kiongozi huyo,pia alimlalamikia rais wa TFF  Leodegar Chillah Tenga kwa kutotimiza ahadi zake kwa klabu ambapo alisema yeye mwenyewe atasimamia hadi kuhakikisha suala la kampuni linaingia kwenye Kamati ya Utendaji, lakini ajabu ameendesha kikao cha Kamati ya Utendaji bila kujadili kampuni.
“Mbaya zaidi ni kwamba, sasa wanakwenda kwenye Mkutano Mkuu (utakaohusisha uchaguzi Mkuu pia) bila ajenda ya kampuni,” alilalamika kiongozi huyo. 
Akiizungumzia Kamati ya Ligi Kuu, kiongozi huyo alisema kwamba ipo kama kivuli na haihusiki na uendeshaji wa Ligi Kuu “Karia anaishi nje ya Dar es Salaam, Ofisa waliyesema ataajiriwa, hadi leo hajaajiriwa. Kazi zote zinafanywa na ofisi ya Sadi Kawemba kama zamani,”alisema. 
Kamati ya Ligi Kuu inaundwa na Wallace Karia (Mwenyekiti), Said Mohamed (Makamu Mwenyekiti), Damas Ndumbaro, Yahya Ahmed, Meja Charles Mbuge, Steven Mguto, Geoffrey ‘Kaburu’ Nyange, Seif Ahmed, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Hemedi Msangi na Henry Kabera (Wajumbe).

Comments