KABURU AZIKA MGOMO WA WACHEZAJI SIMBA SC

Na Dina Ismail
WAKATI mgomo baridi miongoni mwa wachezaji wa Simba ukipatiwa ufumbuzi kwa Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo Geofrey Nyange ‘Kaburu’ kuokoa jahazi, uongozi wa klabu hiyo umemtema katika safari ya Algeria kiungo wake wa kimataifa, Patrick Mutesa Mafisango.
Wachezaji wa Simba waliendesha mgomo wa chini chini kwa karibu siku tatu, wakishinikiza walipwe sh mil. 30 walizoahidiwa na uongozi - iwapo wangeifunga ES Setif ya Algeria, waliyocheza nayo Jumapili iliyopita katika mechi ya awali raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho (CAF) kwenye Uwanja wa Taifa na kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 na kuambulia sh milioni 15 tu.
Habari kutoka katika kambi ya klabu hiyo iliyoko Bamba Beach, Kigamboni jijini Dar es Salaam zinaeleza kuwa Kaburu alikwenda kambini na kuwaongeza shilingi milioni tano na hivyo kuamua kuachana na mgomo huo.
Imeelezwa kuwa pamoja na mgao huo, kulifanyika kikao juzi jioni ambapo wachezaji waliamua kuuzika mgomo huo na kujipanga kikamilifu tayari kwa mchezo wao wa Ligi Kuu Tanzanuia Bara dhidi ya African Lyon utakaopigwa kesho katika dimba la Taifa Dar es Salaam na ile ya marudiano dhidi ya ES Setif itakayopigwa wiki mbili zijazo.
Aidha suala hilo la kudai malipo hayo pia lilipelekea Mafisango kusimamishwa, baada ya kurejea kambini akiwa amelewa na kuanza kumtolea lugha chafu Meneja wa Timu hiyo, Nico Nyagawa, kabla ya kutaka kumpiga Kocha Mkuu, Mserbia Milovan Cirkovic, yote ikiwa ni katika kudai maslahi ya timu hiyo.
Habari zinadai kuwa katika vurumai hiyo, Mafisango aliulalamikia uongozi wa Simba kutojali maslahi ya wachezaji, huku akimshutumu Nyagawa kwa kushindwa kuwatetea pindi walipotaka waongezewe mgao wao. Hata hivyo Mafisango alikuwa hajajua kama tayari wameshaongezwa milioni tano.
Tayari uongozi wa Simba umempa barua ya kumsimamisha kuichezea timu hiyo kwa muda, sambamba na kumtaka ajieleze kutokana na kufanya utovu wa nidhamu kwa  waajiriwa wengine wa klabu hiyo katika kambi ya timu hiyo.
Taarifa iliyotolewa leo na Ofisa Habari wa Simba Ezekiel Kamwaga ilisema kuwa kutokana na utovu huo wa nidhamu, Mafisango hatasafiri na timu kwenda Algeria wiki ijayo itakapoenda kukwaana na Setif ya huko katika mchezo wa marudiano.
“Uongozi tayari umemuandikia barua ya kutaka ajieleze kwa makosa yake na maamuzi kamili yatatolewa mara timu itakaporejea kutoka Algiers,” ilieleza taarifa hiyo.

Comments

  1. YANGA BOMBA - UHURU BRANCHMarch 30, 2012 at 7:06 AM

    Mafisango is a disaster,ni mchezaji mzuri sana lakini hanaga nidhamu,hata azam aliwahi kumtukana kocha mbrazil siku wakiwa safarini kutoka Dodoma kuja Dar kisa yeye na mwenzake nimemsahau jina ila aliwahi kuchezea ashanti akaja simba then ndio akaenda azam nadhani ni kijuso au lidondo walicheza mechi dodoma ilikua jmosi usiku wao wakasema wanaenda disco kocha akawaambia wachezaji timu itaondoka dodoma jpili saa kumi na moja alfajiri hivyo ni bora wachezaji wakapumzika kwa kulala mapema kujiandaa na safari but hamkatazi mtu kutoka ila azingatie muda wa timu kuondoka na kuwahi,kina mafisango wakaenda disco wakachelewa saa kumi na moja kamili kocha akamwambia dereva ondoa gari,kina mafisango ikabidi wakodi teksi kulifukuza basi la timu baada ya kukuta limeondoka,bahati nzuri wakalikuta njiani,basi baada ya kuingia ndani ya basi mafisango akaanza kumporomoshea matusi kocha mbrazil na viongozi wote wa timu na kudiriki kutaka kumpiga,kocha akaapa akifika dar ama yeye aachie ngazi au mafisango aachie,viongozi wa azam wakawa dhaifu kwa mafisango wakaona bora kocha aondoke..huyo ndio mcongoman mafisango ambae amaechukua uraia wa rwanda...ankunywa sana pombe,anavuta sana bangi..!

    mdau wa bomba revere,boston,massachussetts.

    ReplyDelete

Post a Comment