HALI ya hewa ya joto
inaonekana kuwahenyesha wachezaji wa timu ya Es Setiff ya Algeria, ambapo jana
walilazimika kuvua jezi na kuyafakamia maji kila wakati, pale walipokuwa
wakifanya mazoezi kwenye uwanja wa TFF Karume jijini Dar es Salaam.
Ingawa Kocha Geiger Alain na nahodha
wake Slimane Raho, mlinzi mwenye umri wa miaka 36, walisema kuwa hali ya hewa
ya joto haitawafanya kupoteza mchezo wa kwanza wa Kombe la Shirikisho dhidi ya
Simba hapo Jumapili, lakini ni dhahiri kuwa joto limewapa wakatimgumu.
Kila mara wachezaji hao
walikuwa wakipigana vikumbo kuyafakamia maji ya kunywa ambapo mbali ya kunywa
walikuwa wakijimwagia vichwani, katika kile kinachoonekana kuzidiwa na joto.
Ukiondoa tatizo hilo la joto,
lakini maumbile makubwa na uwezo wa wachezaji hao vimewatisha mashabiki
waliofika kwenye uwanja wa Karume kushuhudia mazoezi yao.
Hii ni kutokana na kwamba
asilimia kubwa ya wachezaji hao wana miili mikubwa na mwenye mwili mdogo kwao
ndiye unayeweza kumfananisha na wachezaji wetu tunaoweza kuwahesabu kwamba wana
miili ya wastani.
“La kama miili ndiyo
inayocheza basi Simba wameshafungwa, hawa jamaa wote wana maumbo makubwa ya
kimpira rafiki yangu, halafu wanaweza kumiliki mpira na kuuchezea watakavyo,
kwa kweli mimi sio mtabiri lakini Simba inabidi wajipange,” alisema shabiki
mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Idd Mussa mkazi wa Ilala.
Comments
Post a Comment