JAPAN, AUSTRALIA NA NGUVU YA UVUTANO WORLD CUP 2014

MIAMBA ya soka barani Asia, Australia na Japan zinazoonekana ndizo zenye nguvu kwa sasa zimejikuta zikipangwa pamoja katika ngwe ya mwisho ya kusaka tiketi ya kushiriki fainali zijazo za kombe la Dunia mwaka 2014.
Katika hafla ya upangaji wa makundi zilizofanyika makao makuu ya Shirikisho la soka Asia (ASF) Malaysia, timu hizo zimepangwa kwenye kundi B, kusaka tiketi za kushiriki fainali hizo zitakazofanyika nchini Brazil.
Mbali ya Australia na Japan, kundi B litakuwa pia na timu za Iraq, Jordan na Oman.
Kwenye kundi A kuna waliokwua wenyeji wa fainali za Kombe la Dunia mwaka 2002, Korea Kusini, Iran, Lebanon, Uzbekistan na wenyeji wa fainali za Kombe la Dunia mwaka 2022, Qatar.
Timu mbili za juu kutoka kila kundi zitajikatia tiketi ya kushiriki fainali hizo, wakati timu zitakazoshika nafasi ya tatu kutoka kila kundi zitalazimika kucheza ili kupata timu ya tano itakayoliwakilisha bara hilo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ASF, kinyang’anyiro hicho cha kusaka tiketi hizo kinatarajiwa kuanza kutimua vumbi Juni 3, 2012 na zitamalizika ifikapo Juni 18, 2013.

Comments