Mji wa Morogoro ndiyo utakaokuwa mwenyeji
wa kituo cha Fainali ya Tisa Bora ya Ligi Daraja la Kwanza kuwania nafasi tatu
za kucheza Ligi Kuu ya Vodacom msimu wa 2012/2013 itakayoanza Machi 31 mwaka
huu.
Chama cha Mpira wa Miguu wa
Morogoro (MRFA) ni baadhi ya vyama vya mikoa vilivyokuwa vimeomba kuwa mwenyeji
wa fainali hizo huku chenyewe kikitimiza sehemu kubwa ya vigezo vilivyowekwa na
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Vyama vingine vya mpira wa
miguu vilivyokuwa vimeomba kuwa mwenyeji wa fainali hizo zinazoshirikisha timu
tisa vilikuwa vya mikoa ya Mbeya, Mwanza, Ruvuma na Tabora.
Fainali hizo zitafanyika
kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini humo chini ya usimamizi wa TFF.
Timu zilizofuzu kucheza hatua ya fainali
kutoka kundi A ni Polisi ya Dar es Salaam, Mgambo Shooting ya Tanga na Transit
Camp ya Dar es Salaam. Kundi B ni Mbeya City Council, Mlale JKT ya Ruvuma na
Tanzania Prisons ya Mbeya wakati kundi C ni Polisi ya Tabora, Polisi ya Morogoro
na Rhino Rangers ya Tabora.
Wakati huo huo, mechi kati ya
Temeke United na Small Kids kupata timu moja ambayo itakabaki Ligi Daraja la
Kwanza na nyingine itakayoshuka itachezwa Machi 31 mwaka huu Uwanja wa Jamhuri,
mjini Dodoma.
Kamati ya Ligi ya TFF
iliyokutana Machi 12 mwaka huu iliamua timu hizo ambazo zilishika nafasi ya
mwisho katika makundi yao ya A na B zicheze ili kupata moja itakayoungana na AFC
ya Arusha na Manyoni SC ya Singida kushuka daraja.
AFC na Manyoni tayari
zimeshuka kutokana na kushindwa kucheza mechi zao za ligi hiyo katika hatua ya
makundi. Kwa mujibu wa Kanuni ya 4 ya Ligi Daraja la Kwanza timu tatu zitashuka
daraja.
Baada ya kumalizika hatua ya
kwanza ya ligi hiyo, timu tisa zimefanikiwa kucheza fainali wakati nyingine tano
za Burkina Faso ya Morogoro, Morani ya Manyara, Polisi ya Iringa, Majimaji ya
Songea na Green Warriors (94KJ) ya Dar es Salaam zimefanikiwa kubaki Ligi Daraja
la Kwanza.
Boniface
Wambura
Ofisa
Habari
Shirikisho la
Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
Comments
Post a Comment