ETI YANGA KUIKATIA RUFAA ZAMALEK

BAADA ya kutolewa kwenye ligi ya mabingwa Afrika, klabu ya soka ya Yanga imedai kuikatia rufaa kwa Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) timu ya Zamalek kwa madai ya kukiuka kanuni za Shirikisho hilo kuhusiana na kuingiza mashabiki.
Yanga ilitolewa kwenye michuano hiyo katika raundi ya awali kwa jumla ya mabao 2-1 ambapo katika mechi ya kwanza iliyopigwa nyumbani zilitoka sare ya bao 1-1 kabla ya Yanga kufungwa bao 1-0 ziliporudiana Cairo Misri, wiki iliyopita
Mwenyekiti wa Yanga Lloyd Nchunga amesema kwamba Yanga wanakusudia kufanya hivyo kutokana na ukweli kwamba hawakuruhusiwa kuingiza mashabiki kama sehemu ya kutumikia adhabu yao lakini cha ajabu waliingiza watazamaji zaidi ya 300.
Akienda mbali zaidi Nchunga alisema kuwa cha kusikitisha ni kwamba licha ya Zamalek kukiuka mwongozo huo wa CAF ulidiriki hata kuzuia ujumbe ulioambatana na Yanga Cairo kuingia uwanjani huku wakidai wanaotakiwa kuingia ni wajumbe wa kamati ya utendaji tu.

Comments