DRFA KUTETA NA VILABU KESHO


UONGOZI wa Chama cha Soka Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), kesho unatarajia kukutana na viongozi wa klabu zote za mkoa huo kwa lengo la kujadili mwanzo wa Ligi ya Kanda ya Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa chama hicho, Amin Bakhressa, alisema mkutano huo utafanyika katika ukumbi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuanzia saa tisa alasiri.
Alisema mkutano huo utatoa fursa kwa klabu kujadiliana kwa kina juu ya uendeshaji wa ligi hiyo, ambapo kila timu inatakiwa kuwakilishwa na kiongozi mmoja, huku makatibu wakuu wa vyama vya soka wilaya ya Kinondoni, Temeke na Ilala nao wakiwakilisha wilaya zao katika mkutano huo.
“Viongozi hao wanatakiwa kufika kwenye mkutano wakiwa na usajili wa wachezaji wao, na baada ya mkutano kumalizika, kutakuwa na uhakika wa kuanza ligi yetu mapema,” alisema Bakhressa.
Ligi hiyo itatoa timu tatu kwa ajili ya kuwakilisha mkoa wa Dar es Salaam kushiriki Ligi ya Taifa.
Pia Bakhressa alitoa mwito kwa timu zilizofuzu kushiriki ligi hiyo kulipa mapema ada ya ushiriki sh 75,000, ili kuthibitisha uwapo wao mashindanoni.

Comments