CHIPUKIZI WA KTZ AINGIA KITUO CHA VIPAJI SENEGAL

Mchezaji Sifael Orgenes Mollel (14) amechaguliwa katika mpango wa kukuza vipaji wa Aspire Football Dream ambao uko chini ya Idara ya Ufundi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwenda kituo cha vipaji (centre of excellence) kilichoko Dakar, Senegal.
Mollel kutoka kituo cha Karume alichaguliwa katika mchakato wa mwaka jana uliofanywa na mng’amua vipaji vya soka (scout) kutoka Hispania kwa niaba ya Aspire Football Dreams yenye makao makuu yake Doha, Qatar.
Mpango huo wa Aspire Football Dreams kwa Tanzania una vituo 14 na mchakato wa kusaka mchezaji mmoja kila mwaka uhusisha vituo vyote hivyo ambapo kila kimoja kinatakiwa kuwa na watoto wasiopungua 176.
Mbali ya Karume, vituo vingine ni Kigamboni, Kawe, Tandika, Makongo, Ukonga, Kitunda, Mbagala, Magomeni, Morogoro, Bagamoyo mkoani Pwani na Tabata.
Mollel atakuwa kwenye kituo hicho cha Dakar kwa muda usiopungua miaka mitatu na anatarajiwa kuondoka nchini Machi 6 mwaka huu. Kwa mwaka wa kwanza wazazi wake watalipwa dola za Marekani 2,500, wa pili dola 2,750 na wa tatu dola 3,000.
Mpango wa Aspire Football Dreams ambao unafadhiliwa na mtoto wa Mfalme wa Qatar una vituo viwili vya kuendeleza watoto wenye vipaji (centre of excellence) ambayo viko Doha na Dakar.
Lakini mpango huo unaendeshwa katika nchi 16 tofauti duniani. Nchi hizo ni Cameroon, Costa Rica, Gambia, Ghana, Guatemala, Ivory Coast, Kenya, Mali, Nigeria, Paraguay, Rwanda, Senegal, Tanzania, Thailand, Uganda na Vietnam.

Comments