ANGETILE ASHUKURU WATANZANIA KWA DUA


KATIBU Mkuu wa Shirikisho la soka Tanzania  (TFF), Angetile Osiah
amesema anamshukuru mungu kwa kuwawezesha madaktari bingwa wa upasuaji
nchini India kumpatia matibabu mazuri na hatimaye kurejea salama
nyumbani.

Kabla ya kwenda huko Osiah alilazwa katika kitengo cha Taasisi ya Tiba
ya Mifupa (MOI) katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili,  baada ya
kubainika kuwa ana uvimbe kichwani kwake na hivyo kushauriwa kwenda
nchini India.

Akizungumza na waandishi wa habari leo alisema kwa sasa anaendelea
vizuri ingawa wakati wa zoezi hilo alipata  maumivu makali ya macho
yaliyotokea   wakati akifanyiwa upasuaji  kwani sehemu kubwa ya paji
la uso ilivutwa ili kupata uwiano mzuri wakati wakimshona nyuzi.

Alisema mara baada ya upasuaji huo madaktari walimueleza kuwa  uvimbe
uliota nje ya ubongo na ndiyo kitu cha kushukuru inagwa  ulipoaanza
kugusa ubongo ndio tatizo likaanza na ndio maana hakuwa katika hali ya
kawaida.

Angetile alisema baada ya kumaliza uangalizi maalum aliopewa nchini
humo madaktari hao wamemtaka kwenda katika  hospitali ya Aga Khan
baada ya mwezi mmoja ili kuangalia maendeleo ya afya yake.

“Zoezi la kwenda Aga Khan litakuwa wiki ijayo ila kwa sasa
nashughulikia mapumziko mafupi ya kama wiki mbili hivi ili niweze
kupumzika zaidi,”Alisema Osiah.

Comments