ANGALAU JULAI NAWEZA KURUDI DIMBANI-VIDIC


BEKI wa kati wa Manchester United, Mserbia Nemanja Vidic, amekana taarifa za uwezekano wa kurudi dimbani msimu huu na kuwataka mashabiki wake na wa klabu kumsubiri hadi msimu ujao anakotarajia kuanzia katika mechi za maandalizi ya msimu ‘Pre-Season’.
Ripoti za mwanzini mwa wiki hii zilidai kuwa Nemanja ambaye yuko nje ya dimba tangu mwezi Desemba 2011, alikuwa mbioni kurudi katika mechi ya mahasimu wa Jiji la Manchester, City na United itakayopigwa Aprili 30 kwenye dimba la Etihad.
Hata hivyo Vidic amezikana taarifa hizo na kusisitiza anaweza kuwa tayari kwa kuchezea United angalau hadi mwezi Julai, wakati klabu hiyo itakapokuwa kwenye mechi za maandalizi ya msimu huko Mashariki ya Mbali.
“Uponaji wangu unakwenda vema na ninatarajia kuanza mazoezi tena mwezi Julai mwaka huu. Nafanya kazi ya ziada hivi sasa. Mtarajio ni kwamba ninaweza kurejea dimbani kwa ajili ya msimu ujao.”

Comments