ZAKI AIPOKONYA TONGE MDOMONI YANGA

HISTORIA ilijirudia jana kati ya Yanga na Zamalek, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, baada ya timu hizo kutoka sare ya 1-1 katika mechi ya kwanza, Raundi ya kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mwaka 2000, Mohamed Hussein ‘Mmachinga’ alitangulia kuifungia Yanga kipindi cha kwanza, katika mechi ya kwanza ya Kombe la Washindi, lakini kipindi cha pili Zamalek wakasawazisha na kufanikiwa kupata sare ya 1-1.
Kadhalika, jana mambo yalikuwa hivyo hivyo, Hamisi Kiiza ‘Diego’ alitangulia kuifungia Yanga kipindi cha kwanza, lakini Amr Zaki akaisawazishia Zamalek kipindi cha pili.
Alikuwa ni mshambuliaji wa zamani wa Hull City na Wigan za England, aliyezima ndoto za Yanga kushinda mechi ya kwanza dhidi ya timu za Misri jana.
Nini maana yake? Yanga sasa inatakiwa kwenda kulazimisha ushindi ugenini wiki mbili zijazo kama inataka kusonga mbele katika michuano hii mikubwa Afrika.
Yanga waliuanza vizuri mchezo huo na katika dakika ya nane, mshambuliaji Davies Mwape alikosa bao baada ya kuingia na mpira vizuri kwenye eneo la hatari la Zamalek, lakini akakosa maamuzi hadi akapokonya mpira huo na beki wa wapinzani wao.
Dakika ya 16, Kenneth Asamoah naye alipewa pasi na Kiiza, lakini akapiga nje.
Dakika ya 18, Kiiza alitanguliziwa pasi nzuri na kiungo Haruna Niyonzima, lakini akachelewa na mpira ukadakwa na kipa Abdelwahed El-Sayed.
Baada ya hapo, Zamalek nao wakaanza kushambua na dakika ya 19, mshambuliaji wake, Razak Omotoyossi alifumua shuti kali baada ya shambulizi la kushitukiza, lakini kwa bahati nzuri kipa Shaaban Kado akadaka.
Omotoyossi tena alipiga shuti jingine hafifu, lililotemwa na Kado kabla ya kudaka.
Wageni hao kutoka Misri walimtoa winga Islam Awadh dakika ya 35 na kumuingiza Said Mohamed.
Katika dakika ya 36 Yanga walifanya shambulizi la kushtukiza lililozaa bao. Beki Athumani Iddi ‘Chuji’, aliokoa mpira uliomkuta Nahodha wake, Nsajigwa Shadrack, aliyeambaa kabla ya kutia krosi maridadi, iliyomkuta Kiiza ambaye aliunganisha nyavuni kwa shuti kali.
Baada ya kupata bao hilo, Yanga walionekana kuutawala mchezo huo, huku Zamalek wakionekana kuchanganyikiwa na dakika ya 37 na 39 Mwape alikosa mabao ya wazi kwa kupiga mashuti ‘yasiyo na macho’.
Hadi mapumziko Yanga walikuwa wanaongoza kwa bao hilo moja na kipindi cha pili kilianza kwa kasi, wenyeji wakitaka kuongeza bao na wageni wakisaka la kusawazisha.
Amr Zaki aliingia dakika ya 58 kuchukua nafasi ya Ahmed Samir na nyota huyo wa zamani wa Wigan, alibadilisha kabisa mchezo huo. Zaki alikuwa akimyanyasa atakavyo Chuji, ambaye aliishia kumchezea faulo tu mfungaji huyo bora wa Fainali za Mataifa ya Afrika mwaka 2008.
Bao hilo lilionekana kuwachanganya Yanga na kuanza kucheza hovyo, hivyo kuwapa mwanya Zamalek kutawala mchezo huo.
Hazem Mohamed naye aliingia kuchukua nafasi ya Sabry Raheel dakika ya 66, kuiongezea kasi Zamalek.
Hazem alionekana kuleta usumbufu upande wa kushoto na Mwasyika kushindwa kumdhibiti, huku Zaki akimfanya beki wa kati wa Yanga, Chuji kucheza vibaya eneo la hatari, ingawa mipira yao ya adhabu haikuleta madhara langoni mwa vijana hao wa Jangwani.
Zaki, aliyeingia kutoka benchi aliipatia Zamalek bao la kusawazisha dakika ya 73, baada ya kuwapita mabeki wa Yanga na kupiga mpira uliomshinda Kado na kujaa nyavuni.
Dakika ya 86, Hazem alipiga shuti kali, lakini Kado alidaka na dakika mbili baadaye, Mwape alipiga mpira uliokwenda nje akiwa yeye na kipa wa Zamalek.
Kuona hivyo, Yanga ilimpumzisha Mwasyika na kumuingiza Oscar Joshua dakika ya 87, ili kumdhibiti Hazem, aliyeonekana kumsumbua beki huyo.
Matokeo haya yenye kusononesha kwa wana Yanga, yanamaanisha kocha Mserbia wa klabu hiyo, Kostadin Bozidar Papic ameendeleza rekodi yake ya kushindwa kuing’arisha timu hiyo kwenye michuano ya Afrika.
Hiyo ilikuwa mechi ya tatu Papic anaiongoza Yanga kwenye michuano ya Afrika bila kuondoka na ushindi, baada ya mwaka 2010 kufungwa mechi zote mbili za Ligi ya Mabingwa dhidi ya Saint Eloi Lupopo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Ilifungwa 3-2 Dar es Salaam kabla ya kwenda kumalizwa kwa kupigwa 1-0 Lubumbashi.
Kwa ujumla, Yanga mara ya mwisho kushinda mechi ya Afrika ilikuwa Februari 14, mwaka 2009, ‘ilipoionea’ Etoile d Mironsty ya Comoro.
Ikiwa chini ya Mserbia mwingine, Dusan Savo Kondic, Yanga ilifungwa mechi zote mbili na Al Ahly ya Misri mwaka 2009, ikipigwa 3–0 Cairo na 1-0 Dar esb Salaam katika Ligi ya Mabingwa.
Mwaka jana, Yanga ilicheza Kombe la Shirikisho na kutolewa Raundi ya Kwanza tu na Dedebit ya Ethiopia kwa kufungwa jumla ya mabao 6-4, ikitoa sare ya 4-4 Dar es Salaam kabla ya kwenda kufungwa 2-0 Addis Ababa, wakati ikinolewa na Mganda, Sam Timbe.
Kwa ujumla, Yanga haina cha kujivunia kwenye michuano ya Afrika, zaidi ya kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa 1998, na wakati michuano hiyo ikiitwa Klabu Bingwa Afrika, walicheza Robo Fainali mara mbili 1969 na 1970 na walifika pia Robo Fainali ya Kombe la Washindi mwaka 1996.
Kikosi cha Yanga jana kilikuwa; Shaaban Kado, Shadrack Nsajigwa, Stefano Mwasyika, Athumani Iddi ‘Chuji’, Nadir Horoub ‘Cannavaro’, Juma Seif ‘Kijiko’, Salum Telela, Haruna Niyonzima, Kenneth Asamoah, Davies Mwape/Shamte Ally na Hamisi Kiiza.
Zamalek; Abdelwahed El-Sayed, Mohamed Abdel-Shafy,  Hani Saied, Alexis Enam, Nour El Sayed, Ahmed Samir/Amr Zaki, Sabry Raheel/ Hazem Mohamed,  Mahmoud Fathallah,  Islam Awad/ Said Mohamed, Razak Omotoyossi na Ahmed Hassan.

Comments

  1. YANGA BOMBA-UHURU BRANCHFebruary 18, 2012 at 9:05 PM

    simba ina kipi chakujivunia kiacha azim dewji alpoifikisha fainali ya kombe la caf kwa ahadi hewa ya kia kwa kina binamu yangu hussein marsha na wenzake

    tupe rekodi za mwisho mwiso za simba hivi karibuni imekua ikitolewa katika raundi ya ngapi na kwa kufungwa magoli mangapiusisahau kipigo cha al hoodod kile cha aibu

    MDAU WA BOMBA,BOSTON,USA

    ReplyDelete
  2. Dada sijui kama ni wewe ndio umeandika habari hii au ni mwingine...na kama wewe sasa sijui ni shabiki wa Simba au? mimi kwa kweli soccer la Tanzania si kivile sana, lakini nashangaa a Journalist anaweza andika habari kama hii...kama you did, shame of you...usiwe baised kwa upande mmoja please...andika habari tusome than to focus on one side...it is not fair at all, kwetu sisi wasomaji.
    Mdau
    New York.

    ReplyDelete

Post a Comment