UBAO WA MATANGAZO TOKA TFF

LIGI KUU YA VODACOM 2011/2012

Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inaingia raundi ya 17 kesho (Februari 11 mwaka huu) kwa mechi tano huku ile ya Kagera Sugar na Mtibwa Sugar iliyokuwa ichezwe Februari 12 mwaka huu ikilazimika kusogezwa mbele kwa siku moja.

Mechi za kesho (Februari 11 mwaka huu) ambazo zitaanza saa 10 kamili jioni ni kati ya Simba na Azam (Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam), Toto Africans na Moro United (Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza), Polisi Dodoma na Villa Squad (Uwanja wa Jamhuri, Dodoma), Coastal Union na African Lyon (Uwanja wa Mkwakwani, Tanga) na JKT Oljoro na JKT Ruvu (Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid, Arusha).

Kagera Sugar na Mtibwa Sugar sasa zitacheza Februari 13 mwaka huu kwa vile Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba siku ya Februari 12 mwaka huu umetolewa kwa shughuli za kijamii. Mabadiliko hayo pia yamesababisha mechi kati ya Toto Africans na Mtibwa Sugar iliyokuwa ichezwe Februari 15 mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM Kirumba sasa kuchezwa Februari 16 mwaka huu.

Nayo mechi namba 119 kati ya Yanga na Ruvu Shooting iliyokuwa ichezwe Februari 12 mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam- Chamazi, sasa itafanyika siku hiyo hiyo kwenye Uwanja wa Taifa.

Mechi hiyo imehamishiwa Uwanja wa Taifa kutokana na maombi ya Yanga kwa vile itakuwa ni sehemu ya sherehe za maadhimisho ya miaka 77 tangu kuasisiwa kwa klabu hiyo.

MGAMBO, MORANI KUCHEZA FEB 12

Mechi ya Kundi A ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kati ya Mgambo Shooting ya Tanga na Morani ya Manyara iliyokuwa ichezwe Februari 11 mwaka huu kama ilivyokuwa ile ya Kundi C kati ya AFC ya Arusha na Polisi ya Morogoro zimesogezwa mbele kwa siku moja.

Mabadiliko hayo yametokana na mechi hizo kuingiliana na za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) zinazochezwa kwenye viwanja vya Mkwakwani, Tanga na Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid, Arusha.

Mechi nyingine za FDL zitaendelea kesho (Februari 11 mwaka huu) kama ratiba inavyoonesha. Kundi A, Burkina Faso itakuwa mwenyeji wa Polisi Dar Salaam kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro wakati Temeke United na Transit Camp zitaoneshana kazi Uwanja wa Mabatini mjini Mlandizi.

Kundi B litashuhudia mechi kati ya Mbeya City na Majimaji kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya huku JKT Mlale wakiwa wenyeji wa Small Kids kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea. Nayo Tanzania Prisons itakuwa mgeni wa Polisi Iringa kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Samora.

Mechi ya Kundi C itakuwa moja ambapo Rhino FC itakaikaribisha 94 KJ ya Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.

KOZI YA MAKOCHA NGAZI PEVU YAAHIRISHWA

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeahirisha kozi ya ukocha ngazi pevu (Advanced Level) iliyokuwa ifanyike jijini Dar es Salaam kuanzia Februari 12- 25 mwaka huu.

Kozi hiyo imeahirishwa kwa vile wengi wa makocha walioomba hawakufikia vigezo vilivyowekwa. Vigezo vya msingi vilikuwa mwombaji awe na cheti cha ukocha ngazi ya kati (Intermediate Level), wawe wanafanya kazi hiyo ya ukocha (active) na kuwasilisha cheti cha elimu ya sekondari (kidato cha nne).

Makocha waliokidhi vigezo kwa ajili ya kozi hiyo ni Sospeter Vedasto kutoka mkoani Pwani, Beatus Manga (Temeke), Renatus Shija (Pwani), Ntungwe Selemani (Pwani), William Mamiro (Kinondoni), Ngawina Ramadhan (Temeke), Khatib Mtoo (Temeke), Hamisi Chimgege (Temeke), Selemani Mkumya (Temeke), Idd Cheche (Azam), Mohamed Mayosa (Temeke) na Imam Mbarouk (Shinyanga).
Wawezeshaji wa kozi hiyo ambayo sasa tarehe yake ya kufanyika itatangazwa baadaye ni Mkufunzi wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Jan Poulsen, Mkufunzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu barani Afrika (CAF) ambaye pia ni Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Sunday Kayuni na Mkufunzi wa Chama cha Mpira wa Miguu cha Denmark (DBU), Kim Poulsen.

Comments