STARS YAMPA WAKATI MGUMU MILOVAN

TIMU ya taifa ya soka Tanzania, ‘Taifa Stars’ inayojiandaa kwa ajili ya mchezo wa kuwania kufuzu kwa Kombe la Afrika (AFCON), dhidi ya Msumbiji utakaopigwa Februari 29, imemuweka katika wakati mgumu Kocha wa Simba, Mserbia Milovan Cirkovic, katika maandalizi yake ya mchezo wa marudiano dhidi ya Kiyovu ya Rwanda.
Mchezo huo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika (CAF), unatarajiwa kupigwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, kati ya Machi 3-4 mwaka huu, baada ya ule wa awali uliopigwa Kigali mwishoni mwa wiki na kumalizika kwa sare ya bao 1-1.
 Ofisa Habari wa Simba  Ezekiel Kamwaga amesema ugumu huo kwa Milovan, unatokana na kulazimika kupangua programu zake za mazoezi yanayoanza leo, baada ya nyota wake tisa kuitwa Stars.
Alisema nyota wao waliobaki baada ya wale wa Stars ni 18, ambao leo wataanza mazoezi baada ya kupumzika siku mbili.
Wachezaji wa Simba walioitwa Stars, ambayo jana ilianza kambi ni Jonas Gerald, Juma Kaseja, Masoud Cholo, Juma Nyoso, Juma Jabu, Kelvin Yondani, Shomari Kapombe, Mwinyi Kazimoto na Uhuru Selemani.

Comments