SIMBA YATOKA 1-1 NA KIYOVU SPORT

NA ASHA KIGUNDULA, KIGALI
SIMBA leo imelazimishwa sare ya kufungana 1-1 na Kiyovu Sport ya Rwanda, katika mechi ya kwanza ya Raundi ya Kwanza, Kombe la Shirikisho Afrika, kwenye Uwanja wa Nyamirambo mjini Kigali.
Wekundu wa Msimbazi ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao kupitia kwa kiungo wake mahiri, Mwinyi Kazimoto Mwitura, katika dakika ya 43.
Kazimoto alifunga bao hilo kwa ustadi mkubwa, baada ya kupokea pasi nzuri ya kiungo chipukizi anayekuja juu, Shomari Kapombe.
Hadi mapumziko, Simba ilikuwa mbele kwa bao hilo moja, lakini kipindi cha pili wenyeji walicharuka na kusaka bao la kusawazisha.
Juhudi zao zilizaa matunda dakika ya 87, Yussuf Ndayishimiye alipounganisha kimiani pasi ya Simon Okwi.  
Simba inayofundishwa na Mserbia Milovan Cirkovick, sasa inahitaji hata sare ya bila kufungana kwenye mchezo wa marudiano wiki mbili baadaye mjini Dar es Salaam ili kusonga mbele.
Simba iliyoshuka dimbani jana ikiwa inaongoza Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na katika mechi zake nne za mzunguko huu wa pili, imeshinda tatu dhidi ya Coastal Union 2-1, JKT Oljoro 2-0 na Azam FC 2-0 na kufungwa moja 1-0 na Villa Squad, jana iliizidi katika kila idara Kiyovu.
Ikifanikiwa kuitoa Kiyovu, Simba itamenyana na Entente Setif ya Algeria.
Mwaka jana, Simba ilicheza Ligi ya Mabingwa na katika Raundi ya Kwanza iliitoa Elan Mitsoudje kwa jumla ya mabao 4-2 na Raundi ya Pili ikatolewa na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kwa jumla ya mabao 6-3.
Hata hivyo, Simba ilirudishwa na CAF mashindanoni baada ya kushinda rufaa waliyomkatia beki wa Mazembe, Janvier Besala Bokungu, aliyevunja mkataba kinyume cha taratibu na klabu ya Esperance ya Tunisia.
Simba ilicheza mechi maalum ya mkondo mmoja na Wydad Casablanca ya Morocco mjini Cairo, kuwania kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa nchini Misri na kufungwa mabao 3-0, hivyo kuangukia kwenye hatua ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho Afrika, ambako ilitolewa na DC Motema Pembe ya DRC kwa mabao 2-1.
Simba ndiyo klabu ya Tanzania yenye rekodi nzuri zaidi katika michuano ya Afrika, ikiwa imewahi kufika Fainali ya Kombe la CAF mwaka 1993, kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2003, wakiwatoa wapinzani wa Yanga mwaka huu, Zamalek na pia wakati michuano hiyo ikiitwa Klabu Bingwa Afrika walicheza Nusu Fainali mwaka 1974.
Kikosi cha Simba jana kilikuwa; Juma Kaseja, Said Nasor ‘Cholo’, Juma Jabu, Juma Nyosso, Kelvin Yondani, Shomari Kapombe/ Uhuru Suleman, Ramadhani Singano ‘Messi’, Mwinyi Kazimoto, Patrick Mafisang, Emanuel Okwi na Felix Sunzu/Victor Costa.

Comments