KLABU ya Zamalek, imetupilia mbali ombi
la timu ya Yanga ya Tanzania ,
kutaka kusiwepo mechi ya marudiano baina yao
iliyopangwa kupigwa mjini hapa kati ya Machi 2 hadi 4, wakihofia hali ya
usalama.
Kwa mujibu wa ratiba ya Shirikisho la
Soka Afrika (Caf), mechi hiyo ya marudiano ya hatua ya awali ya Ligi ya
Mabingwa Afrika, itapigwa wiki mbili baada ya ile ya kwanza itakayochezwa
Februari 18, kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam .
Awali, uongozi wa Yanga uliandika barua
Caf, kupitia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuomba uwepo wa mechi moja tu
ya kuamua timu ya kusonga mbele katika michuano hiyo, hivyo kufuta mechi hiyo
ya marudiano.
Jumanne wiki hii, TFF lilituma ombi hilo Caf, ikitambua kuwa, uamuzi wa jambo hilo
ungetegemea matakwa ya Zamalek, iwe kuchezwa mechi moja au pambano hilo kuhamishiwa nchi
nyingine kwa sababu za kiusalama.
Yanga, wametaka mechi moja, wakisita
kwenda Cairo ,
Misri kwa mechi ya marudiano, baada ya kutokea vurugu za mashabiki katika mechi
ya Ligi Kuu kati ya Ahly na El Masry iliyopigwa kwenye Uwanja wa Port Said.
Katika mechi hiyo, ambayo iliisha kwa
Ahly kufungwa mabao 3-1, mashabiki wa El Masry, walivamia uwanja na kuanza kushangilia
wakirusha fataki na chupa za maji dhidi ya mashabiki wa Ahly, ambao nao
walijibu mapigo.
Hali hiyo ikazusha mapigano na
mkanyagano mkubwa hadi kusababisha vifo vya mashabiki takriban 74 na wengine
1,600 kujeruhiwa, hivyo nchi hiyo kuingia kwenye maombolezo ya siku tatu.
Kwa mujibu wa Kocha Msaidizi wa Zamalek,
Ismail Youssef, bosi wake (Hassan Shehata), amekataa kucheza mechi moja na kama vipi, wapo tayari mechi hiyo ipigwe bila mashabiki
mjini hapa.
“Kocha (Hassan) Shehata amesisitiza
kuwa, mechi ya marudiano dhidi ya Yanga, lazima ichezwe Misri, hata kama itakuwa bila mashabiki kwa sababu za
kiusalama,” alisema kocha huyo msaidizi
kupitia mtandao.
Zamalek, ambayo mwaka jana iliamriwa
kucheza mechi mbili za nyumbani bila mashabiki, kutokana na vurugu za mashabiki
wake.
Zamalek wametoa msimamo huo, huku Caf
ikitarajia kujadili vurugu hizo kesho Jumamosi, kuangalia hatua za kuchukua
dhidi ya waliohusika kwa namna moja au nyingine na maafa hayo makubwa zaidi
katika soka ya Misri.
Comments
Post a Comment