MECK SADICK AFUNIKA AIBU SHEREHE ZA YANGA


MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam ameifutia aibu klabu kongwe ya Yanga ya jijini Dar es Salaam baada ya hafla maalumu ya kuichangia katika maadhimisho ya miaka 77 tangu kuanzishwa kwake kudoda kwenye Hoteli ya Peacock.
Katika hafla hiyo iliyokuwa imepangwa kuanza majira ya saa 1:00, uongozi wa Yanga uliwaalika wadau mbalimbali wakiwamo viongozi wa serikali na wafanyabiashara wakubwa, lakini mahudhurio yalikuwa hafifu.
Hadi muda wa kuanza shughuli  habari za uhakika kutoka ndani ya klabu hiyo zinaeleza kuwa kulikuwa hakuna hata kiongozi mmoja, isipokuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki, ambaye alikuwa mgeni rasmi.
“Yaani RC aliingia ukumbini kama saa 1:30 hivi, lakini kulikuwa hakuna kiongozi hata mmoja, hivyo kuonekana mgeni rasmi ndiyo mkaribisha wageni,” kilisema chanzo hicho na kuongeza:
“Kutokana na maandalizi hafifu ambayo hayaendani na miaka 77 ya Yanga, mbali na RC, viongozi wengine wakamwalika Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara, hivyo mambo kuzidi kuingiliana.
Inaelezwa kuwa hali ilizidi kuwa mbaya wakati mnada wa vitu mbalimbali ulipoanza ambapo kutokana na walengwa wengi kuingia mitini, mauzo yalidoda, hadi pale RC Sadiki, alipookoa jahazi kwa kununua picha ya Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume kwa sh 1,750,000.
“Yaani si viongozi wala hao walioalikwa, hakuna chochote walichokifanya, yaani ni aibu aibu, walileta jezi kibao lakini hakuna aliyenunua zaidi ya jezi tatu kwa sh laki moja kila moja,” alisema mtoa habari huyo na kubainisha kuwa
Kamati ya Utendaji ndiyo kila kitu Yanga, lakini viongozi hawakupewa taarifa juu ya suala hilo na wao hawakuelewa chochote, ndiyo maana walikuwa wanashangaa tu.
“Yaani bila ya Mkuu wa Mkoa Saidi Meck Sadiki ambaye alitarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo kununua picha ya aliyekuwa Rais wa awamu ya kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume, ingekuwa aibu tupu,” alisisitiza.


Mwisho

Comments