KIDUM KUKAMUA DAR ALIVE JUMAPILI


Na Mwandishi Wetu
MKALI wa miondoko ya zouk na pop, Kidum anatarajia kufanya shoo kali keshokutwa Jumapili wenye Ukumbi wa Dar Live, Mbagala Zakhem jijini Dar es Salaam. 
Pamoja na burudani yam kali huyo, pia kutakuwa na mchujo wa pili wa shindano la Vaa, Imba na Cheza kama Rihanna ambalo mshindi wake atazawadiwa Sh milioni 10. 
Kidum raia wa Burundi ambaye kwa sasa ni msanii namba moja wa miondoko hiyo nchini Kenya anatamba na nyimbo mbalimbali na amejigamba kufunika siku hiyo kwenye ukumbi wa Dar Live. 
Baadhi ya nyimbo ambazo anatamba nazo ni pamoja na Karibia ft Nameless, Haturudi nyuma ft Juliana Kanyomozi, Nitafanya ft Lady Jaydee, Urugendo,AmosoziNgwinoNumber, 
 
Kidum atafanya shoo yake hiyo kwa kushirikiana na bendi yenye wanamuziki zaidi ya sita ambao amesafiri nao kutoka jijini Nairobi, Kenya yaliko makazi yake. 
Pamoja na mkali huyo wa Afrika Mashariki, kwa hapa nyumbani upande wa miondoko hiyo kutakuwa na Linex ambaye ataonyesha makali yake na nyimbo kadhaa ukiwemo ule wa ‘Mama Halima’. 
Kwa upande wa dansi, mkongwe Hassan Bitchuka atawaongoza Sikinde Bend kuonyesha walichonacho na kuwakonga mashabiki wao.
Miondoko ya pwani itakuwa chini wa malkia wa mipasho, Khadija Omar Kopa ambaye atafanya mambo akiwa na kundi la TOT Taarab. 
Mratibu wa Burudani wa Dar Live, Juma Mbizo amesema siku hiyo milango itafunguliwa mapema, “Asubuhi mpaka mchana kama kawaida watoto watapata nafasi ya kucheza na kuogelea. 
“Shoo itakuwa bab kubwa, Linex amesema amejipanga kumkabili Kidumu na atafanya ‘sapraizi’ kwa kutambulisha wimbo wake mpya alioimba na Diamond,” alisema Mbizo.

Comments