CHELSEA BALAA JUU YA BALAA, YAPIGWA 3-1 ITALIA


Mshambuliaji wa Napoli, Ezequiel Ivan Lavezzi (katikati) akishangilia bao lake dhidi ya Chelsea usiku huu katika Ligi ya Mabingwa Ulaya Uwanja wa San Paolo. Napoli ilishinda 3-1.

NAPOLI usiku huu imepata ushindi mtamu nyumbani katika mechi ya kwanza, hatua ya 16 Bora Ligi ya Mabingwa Ulaya wa mabao 3-1 dhidi ya Chelsea ya England kwenye Uwanja wa San Paolo, Napoli. Hadi mapumziko, Chelsea walikuwa nyuma kwa mabao 2-1.
Chelsea walikuwa kupata bao dakika ya 27 mfungaji Juan Mata, lakini dakika ya 39, Ezequiel Ivan Lavezzi akasawazisha kwa pasi ya Edinson Roberto Cavani kabla ya Cavani mwenyewe kupiga la pili, dakika ya pili ya muda wa nyongeza baada ya kutimu kwa dakika 45 za kipindi cha kwanza, kwa pasi ya Inler.
Kipindi cha pili, timu hiyo ya zamani wa gwiji wa soka Argentina, Diego Maradona iliingia na moto na katika dakika ya 65, Lavezzi alipiga bao la tatu akiunganisha pasi ya Cavani aliyekuwa mwiba mchungu kwa mabeki wa Chelsea.
Chelsea sasa watahitaji ushindi wa mabao 2-0 au zaidi nyumbani Stamford Bridge ili wafufue matumaini ya England kutwaa taji hilo msimu huu.
Arsenal tayari inachungulia mlango wa kutokea kwenye michuano hiyo, baada ya kufungwa 4-0 na AC Milan katika mchezo wa kwanza wa hatua hiyo mjini Milan wiki iliyopita.
Vigogo wengine wa England, Manchester City na Manchester United wameangukia kwenye Europa League.
Katika mchezo uliotangulia, Pontus Wernbloom alifunga katika dakika ya tatu ya muda wa nyongeza na kuiwezesha timu yake CSKA Moscow kupata sare ya 1-1 na Real Madrid katika mchezo wa kwanza hatua ya 16 Bora Ligi ya Mabingwa Ulaya usiku huu.
Wernbloom alikutana na mpira ambao ulimbabatiza beki wa Madrid, Alvaro Arbeloa na kuusukuma nyavuni.
Katika mchezo huo uliofanyika kwenye Uwanja wa Luzhniki mjini Moscow, Urusi, Mreno Cristiano Ronaldo aliifungia Real Madrid bao la kuongoza dakika ya 28, hilo likiwa bao lake la 36 msimu huu.
Mechi ya marudiano baina ya timu hizo itapigwa Hispania Machi 14, mwaka huu.

Comments

Post a Comment