TAARIFA
KWA UMMA
Idara ya Sanaa ya Chama
Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) imepokea taarifa kwa vyombo vya habari
iliyotolewa kuhusu mapatano baina ya Mheshimiwa Joseph Mbilinyi (Mb) na
Rugemalira Mutahaba.
Taarifa hiyo ya tarehe
21 Februari 2011 imeeleza pamoja na mambo mengine kuwa pande mbili hizo
zimekubaliana kushirikiana kufanikisha haki na jitihada za kuinua maslahi ya
wasanii. Aidha, pande mbili hizo zimekubaliana kufanya jitihada za pamoja
kuunganisha vyama vya wasanii vya TUMA na TFU ili kutetea maslahi ya wasanii
wakiwa na umoja zaidi.
Idara ya Sanaa ya
CHADEMA inatambua kwamba makubaliano hayo ni hatua ya kwanza kwa pande hizo
mbili na wadau wanaoshirikiana nao katika jitihada za kuboresha sanaa nchini hususan
ya muziki wa kizazi kipya; hivyo hatua zaidi zinapaswa kufuata.
Idara ya Sanaa ya
CHADEMA inampongeza Mbilinyi maarufu kama Sugu
ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Habari, Vijana na Utamaduni kwa kuendeleza
harakati za kupigania haki za wasanii ndani na nje ya bunge hali ambayo imeibua
mjadala na hatimaye kufikiwa kwa makubaliano hayo. Kusainiwa kwa makubaliano
hayo ya kuunganisha nguvu kumedhihirisha kwamba ‘palipo na msuguano pana
mwendo’ (where there is friction, there is movement).
Kwa kuwa mashahidi
katika mapatano hayo ni Waheshimiwa Dr. Emmanuel Nchimbi (Mb) ambaye pia ni
Waziri wa Habari, Vijana na Utamaduni na Tundu Lissu (Mb) ambaye pia ni Waziri
Kivuli wa Sheria na Katiba; idara ya sanaa inatarajia kuwa kwa misingi ya
makubaliano yaliyofikiwa yanayohusu hatua za kiserikali na kibunge nguvu za
ziada zitaunganishwa kwa ajili ya kufanikisha utekelezaji.
Idara ya Sanaa ya
CHADEMA inatarajia kwamba kwa makubaliano hayo sasa wadau wote wataunganisha
nguvu za pamoja ili wasanii waweze kuwakilishwa ipasavyo na chama chao chenye
kutambuliwa rasmi na Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA).
Aidha, idara ya sanaa
ya CHADEMA inatambua kuwa kufuatia mapatano hayo sasa serikali inapaswa kuanza
utaratibu wa kuhakikisha kwamba vifaa vya studio vilivyotolewa na Rais Jakaya
Kikwete inawekwa chini ya chombo ambacho wasanii wengi wataweza kunufaika.
Idara ya Sanaa ya chama,
inatambua kwa mujibu wa katiba ya CHADEMA chama kinaamini katika falsafa ya
nguvu ya umma, hivyo jitihada zozote za kuunganisha nguvu za pamoja kwenye mambo
ya kudai haki za msingi ni suala linalohitaji kuungwa mkono. Aidha, kwa mujibu
wa katiba ya CHADEMA chama kinaamini
kwenye itakadi ya mrengo wa kati inayotaka pamoja na mambo mengine fursa
kutolewa kwa wote zenye kuhakikisha pamoja na mambo mengine vipaji vya vijana
vinaendelezwa.
Hivyo, Idara ya Sanaa
ya CHADEMA itaendelea kufuatilia hatua zinazochukuliwa za kuunganisha nguvu za
pamoja kutetea haki za wasanii ikishirikiana na Waziri Kivuli wa Habari, Vijana
na Utamaduni, Joseph Mbilinyi na wadau wengine.
Imetolewa tarehe 24 Februari 2012 na:
Fulgence Mapunda
(Mwana-Cotide)
Afisa wa Idara ya Sanaa
Comments
Post a Comment