ARSENAL YATOLEWA KOMBE LA FA, CHELSEA MGUU NJE, MGUU NDANI

WAZEE wa gundu, Arsenal jana walipigwa mabao 2-0 na Sunderland na kutolewa kwenye Raundi ya Tano ya Kombe la FA, hivyo kujitengenezaea mazingira ya kumaliza msimu wa saba bila taji lolote.
Arsenal inayozidiwa pointi 17 na vinara wa Ligi Kuu England, Manchester City, pia walipigwa mabao 4-0 katika mechi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, hatua ya 16 Bora na AC Milan wiki iliyopita mjini Milan.
Mabao yaliyowaua The Gunners jana yalitupiwa kwenye kamba nyembamba na Richardson aliyeunganisha mpira wa adhabu uliopigwa na Sebastian Larsson dakika ya 40 wakati Larsson mwenyewe akapiga la pili zikiwa zimesalia dakika 12, akiuwahi mpira uliorudi baada ya kumgonga winga wa Arsenal, Alex Oxlade-Chamberlain na kuutumbukiza nyavuni.
Thierry Henry—aliyefunga bao la ushindi katika ushindi wa 2-1 kwenye Ligi Kuu wiki iliyopita hakuwepo kabisa Arsenal jana. Alimaliza muda wake wa kucheza kwa mkopo kwenye klabu yake hiyo ya zamani, akitokea New York Red Bulls Alhamisi.
Chelsea ilitoka 1-1 na Birmingham na zitalazimika kurudiana.
Timu nyingine ya Daraja la Kwanza, Leicester iliitoa Norwich kwa kuichapa mabao 2-1, Everton iliifunga Blackpool 2-0 na Bolton iliitandika 2-0 Millwall.

Comments