ALI KIBA, ROMA KUPAMBA VAA, IMBA, CHEZA KAMA RIHANNA DAR LIVE J'2

WAKATI shoo ya Family Day ikiendelea kunoga Jumapili hii ndani ya
Ukumbi wa Kisasa wa Dar Live, Shindano la Vaa, Imba, Cheza kama
Rihanna litazidi kutimua kasi huku warembo 12 wakichuana vikali
kuwasaka watano watakaoingia fainali.
Siku hiyo wasanii Ali Kiba na Roma watakonga nyoyo za umati
utakaojitokeza katika ukumbi huo uliopo maeneo ya Mbagala, Zakhem
jijini Dar es Salaam.
Kiba ambaye ni mara chache kufanya shoo hapa nyumbani, anafanya vizuri
na nyimbo kama ‘Dushelele’, huku wengi wakitarajia kumuona akiimba
zile za zamani ‘Mac Mugga’ na ‘Cidelerra’.
Pia kutakuwa na burudani nyingine kutoka kwa bendi ya Extra Bongo,
huku Jahazi Modern Taarab inayoongozwa na Mzee Yusuf wakiotumbuiza kwa
upande wa miondoko ya pwani.
Ishu kubwa itakuwa ni kuwapata warembo watano watakaofanikiwa kutinga
hatua ya fainali kwani mchuano uliopo ni mkali na kila mmoja
amejipanga vyema kuhakikisha hakosi kuingia katika hatua hiyo.
Mwalimu wa warembo hao, Dotto Villet ‘Spencer’ alisema: “Nahisi
itakuwa vigumu kuwapata warembo watano kwani viwango vyao havipishani
sana, kila mmoja amejiandaa vizuri na shindano linazidi kuvuta hisia
za watu wengi.”
Akizungumzia shindano hilo lilivyoanza, Mratibu wa Burudani wa Ukumbi
wa Dar Live, Juma Mbizo, alisema: “Tulianza na washiriki zaidi ya 60
tukawafanyia mchujo wa kwanza katika Hoteli ya The Atriums, wakabaki
30.
“Hao 30 wakaingia kambini Sinza, Mapambano katika Ukumbi wa Royal Tree
Social Hall, tukaendelea na mchujo uliofanyika Dar Live na kubakiza
washiriki 20. Hao 20 waliendelea na mazoezi ambapo walichujwa na
kubaki 12 ambao tupo nao mpaka sasa.
“Keshokutwa (Jumapili) watachujwa na kubaki watano watakaoingia
fainali, katika hao atapatikana mmoja atakayeondoka na kitita cha
shilingi milioni 10. Wengine waliofikia fainali wataondoka na kifuta
jasho. Shoo itaanza saa 12:00 jioni hadi usiku wa manane na kiingilio
kitakuwa Sh 5,000 kwa wakubwa na 2,000 kwa watoto,” alisema Mbizo.

Comments