YANGA WAMUANGIKIA MOSHA

ALIYEWAHI kuwa Makamu Mwenyekiti wa klabu ya soka ya Yanga, Davis Mosha (pichani) amesema yupo tayari kuisaidia timu hiyo kama alivyoobwa lakini ameutaka uongozi wa klabu hiyo umwandikie barua ya dokezo la mahitaji ambayo wanahitaji kutoka kwake.
Hatua hiyo inafuatia hivi karibuni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano na Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya klabu hiyo Mohammed Bhinda kumuomba Mosha kuhudhuria mazoezi ya timu hiyo yaliyokuwa yakifanyika kwenye mazoezi kwenye Uwanja wa Loyola Mabibo,Dar es Salaam, kwa lengo la kuwapa motisha wachezaji hao ili waweze kufanya vema katika maandalizi ya mechi zao na hasa ile ya klabu bingwa ya Afrika dhidi ya Zamalek ya Misri itakayopigwa Februari 2 na 4 mwaka huu.
Hata hivyo kutokana na majukumu aliyokuwa nayo Mosha alishindwa kutokea siku hiyo, hivyo kuutaka uongozi wa klabu hiyo umwandikie mahitaji ambayo wamepungukiwa ili aweze kujipanga ni kwa kiasi hani atawasaidia.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mosha alisema kuwa akiwa kama mwanachama na mpenzi wa timu hiyo ameguswa na ombi hilo hivyo ameahidi kutoa msaada pale atakapoweza lakini kwanza uongozi umwandikie dokezo la mahitaji.
“Nafahamu kuwa timu yetu inakabiliwa na mchezo mgumu wa klabu bingwa Afrika dhidi ya Zamalek, hivyo tunatakiwa kuisaidia timu yetu ili kuhakikisha inafanya maandalizi mazuri na wachezaji wanakuwa na ari ya ushindi, kitendo cha uongozi kuniomba niwape motisha wachezaji na kisha kukaa kimya haileti picha nzuri inaonekana kama walikuwa wananisanifu,” alisema Mosha.
Mosha aliongeza kuwa bado hajakata tamaa kuisaidia timu hiyo na endapo viongozi watamwandikia dokezo la mahitaji ya timu hiyo hatosita kusaidia kwa kile atakachojaliwa kwa nafasi yake.

Yanga kwa sasa inakabiliwa na ukata wa hali ya juu ambapo kocha mkuu wa timu hiyo, Kostadin Papic amedaipamoja na kutoa taarifa kwa uongozi bado umekaa kimya na kusema kuwa hatua hiyo inaweza kuchangia timu kufanya vibaya katika mechi yake na Zamalek hivyo asilaumiwe kwa matokeo mabaya ya timu hiyo.

Hata hivyo hivyo hali hiyo inachangia na baadhi ya viongozi kuwa wababaishaji hali iliyopelekea baadhi ya wadu ambao wamekuwa wakitoa misaada katika klabu hiyo kuajiweka kando.

Comments