WADAU WAIPONGEZA BASATA KURATIBU MATUKIO YA SANAA



Rais wa Shindano la Miss Utalii, Gideon Chipungahelo (Katikati) akiongea na wadau wa Sanaa kuhusu miaka mitano ya shindano hilo kwenye Jukwaa la Sanaa linalofanyika kila wiki makao makuu ya BASATA. Kulia ni Mkurugenzi wa Utawala na Fedha wa Miss Utalii Aboubakar Omar na Mkuu wa Kitengo cha Matukio wa BASATA, Omary Mayanga, 

Na Mwandishi Wetu
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limepongezwa na wadau wa Sanaa kwa juhudi zake katika kusimamia na kuratibu matukio mbalimbali ya Sanaa hapa nchini na kuyafanya kudumu.
Pongezi hizo zimetolewa wiki hii na wadau wa Sanaa wakati wakichangia mjadala uliohusu miaka mitano ya shindano la miss utalii na sanaa ya urembo nchini kwenye Jukwaa la Sanaa linalofanyika kwenye Ukumbi wa BASATA uliopo Ilala, Sharif Shamba.
Akizungumza wakati akieleza historia za shindano hilo, Rais wa Miss Utalii, Gideon Chipungahelo alisema kuwa, BASATA imekuwa bega kwa bega na shindano hilo katika kuhakikisha miongozo na kanuni mbalimbali za kuendesha mashindano zinafuatwa na kusisitiza kuwa, hiyo ndiyo sababu ya shindano hilo kuweza kupata baadhi ya mafanikio ya ndani na nje ya nchi.
“Naishukuru Serikali na BASATA, kila mara wamekuwa wakitoa maelekezo na miongozo ambayo imelifanya shindano hili kufikia mafanikio haya ingawa kumekuwa na changamoto kadhaa hasa za kukosa wadhamini” alisistiza Chipungahelo.
Aliongeza kuwa, BASATA imekuwa mara kwa mara ikikutana na kamati ya miss utalii na kuipa maelekezo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufanya tathimini na wadau wa sanaa ya urembo ambao wamekuwa wakitoa michango ya kuliboresha shindano hilo.
Awali wadau wa Jukwaa la Sanaa walipata wasanii wa kutoa maoni na ushauri kuhusu shindano la miss utalii ambapo walitoa changamoto kadhaa na kushauri jinsi ya kuzitatua na kulifanya shindano hilo lizidi kusonga mbele
“Shindano hili ni zuri na ni kiungo kizuri cha kukuza utalii kama waandaaji watalisimamia vizuri, ni vema kuwa na kamati  maalum ya uendeshaji inayowajibika na wadhamini waone umuhimu wa kulifadhili shindano hili” alishauri Mzee Mwali Ibrahim ambaye ni mwandishi wa habari za uchumi wa gazeti la Majira.
Aliishauri kamati ya miss utalii kuliunganisha shindano hilo na maendeleo ya sekta ya sanaa nchini.
 

Comments