TUTA LAIOKOA YANGA KUZAMA

MWANASKA bora wa Uganda 2011, Hamisi Kiiza ‘Diego’ jana aliinusuru Yanga kuzama katika mchezo wa kwanza wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Morio United, alipoifungia bao la kusawazisha na kufanya sare ya 2-2 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Matokeo hayo yameiwezesha Yanga kufikisha pointi 28 sawa na Simba, lakini Wanajangwani hao wakiwa wamezidiwa kwa wastani mzuri wa mabao na watani wao hao wa jadi waliopo kileleni.
Yanga ikiwa imecheza mechi 14, ina wastani wa mabao tisa dhidi ya 13 ya Simba iliyoshuka dimbani mara 13.
Wekundu wa Msimbazi wao watarusha karata yao ya 14 Jumatano kwa kupambana na Coastal Union kwenye Uwanja wa Taifa, huku Azam ikipepetana na African Lyon kwenye Uwanja wa Chamazi, Mbagala.
Katika mchezo wa jana, Yanga ndio walioanza kufunga bao dakika ya 43 kupitia kwa Mghana Kenneth Asamoah aliyemalizia krosi kutoka kwa Mnyarwanda Haruna Niyonzima.
Moro Utd walisawazisha bao hilo dakika ya 49 kupitia kwa Benedict Ngassa aliyefunga kwa kwa kichwa kutokana na pasi ya Kelvin Charles.
Kuingia kwa bao hilo, kuliiongezea nguvu Moro na kuzidisha mashambulizi langoni mwa Yanga ambapo dakika 73, timu hiyo iliongeza bao la pili lililofungwa na Simon Msuva alipoiwahi pasi ndefu ya Ngassa iliyomshinda Nadir Haroub ‘Cannavaro’ alipotaka kuiwahi.
Dakika tano baadaye, Yanga walisawazisha kwa mkwaju wa penalti iliyopigwa na Hamis Kiiza baada ya Meshack Abel kuunawa mpira eneo la hatari.
Katika mchezo huo, Yanga walicheza pungufu kwa dakika 50 baada ya nahodha wao, Shadrack Nsajigwa kuonyeshwa kadi nyekundu kwa kosa la kumpiga kiwiko Ngassa.
Hivyo ilibidi Nurdin Bakari achukue nafasi yake na Omega Seme aliyechukua nafasi ya Asamoah, akacheza kama kiungo wa pembeni, washambuliaji wakabaki Davies Mwape na Kiiza.
Mabingwa hao wa Bara, walitawala kipindi cha kwanza, lakini kutolewa kwa Nsajigwa, kulionekana kuiathiri safu ya ulinzi ya timu hiyo na kutoa mwanya kwa Moro kutikisa nyavu.
Yanga ndio walioanza kulifikia lango la Moro ambapo dakika ya 10, Asamoah alikosa bao baada ya kupoteza pasi nzuri ya Kiiza kwa shuti lake kwenda pembeni ya goli.
Dakika 26, timu hiyo ilikosa tena bao kutokana na mpira wa adhabu ndogo iliyopigwa na Stephano Mwasika na kumkuta Kiiza aliyepiga kichwa hafifu kilichotoka nje.
Dakika 30, Moro nayo ilifanya makosa kwa kushindwa kufumania nyavu baada ya Tumba Swedi kupiga nje mpira wa adhabu ndogo nje ya 18.
Katika kipindi cha pili dakika ya 48, Moro ilimtoa beki wa zamani wa Yanga, Fred Mbuna na kumwingiza Simon Msuva.
Dakika ya 52, Mwape alikosa bao akiwa na kipa na dakika ya 67, timu zote zilifanya mabadiliko kwa Moro kumtoa Kelvin na kuingia Sultan Kasikasi, wakati Yanga walimtoa Mwape na kuingia Jerry Tegete.
Dakika 85 Moro ilimtoa Lambele Jerome na kuingia Rajab Zahir ambapo mabadiliko hayo, hayakubadili matokeo ya mchezo huo uliochezeshwa na mwamuzi Hashim Abdalah wa Dar es Salaa..
Akizungumzia mchezo huo, kocha wa Yanga, Kostadin Papic, alisema kuwa hajafurahishwa na matokeo hayo kwani wachezaji wake walikosa nafasi nyingi, huku akilalamikia kadi nyekundu aliyoonyeshwa Nsajigwa ikiipunguzia kasi timu yake.
Kwa upande wake, kocha wa Moro, Hassan Banyai, aliwapongeza wachezaji wake akitamba kuwa kila mechi ya ligi hiyo, watacheza kama fainali.
YANGA: Shaaban Kado, Shadrack Nsajigwa, Stephano Mwasika, Bakari Mbegu, Nadir Haroub, Juma Seif, Nurdin Bakari, Haruna Niyonzima, Davies Mwape, Kenneth Asamoah na Hamisi Kiiza.
MORO:Jackson Chove, Erick Mawala, Salum Kanon, Tumba Swedi, Meshack Abel, Gidion Seppo, Bennedict Ngassa, Hilal Bingwa, Lambele Jerome, Kelvin Charles  na Fredy Mbuna
Katika mechi nyingine za ligi hiyo za jana, Mtibwa Sugar ikiwa katika uwanja wake wa Manungu, Turiani, ilipokea kipigo cha bao 1-0 kwa Oljoro JKT kwa bao lililofungwa na Meshack Mlembele dakika ya 90, huku Villa Squad ikichabangwa mabao 4-2 na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Chamazi.
Kwenye Uwanja wa Mlandizi, Pwani, Ruvu Shooting waliichapa Toto African ya Mwanza mabao 2-0.
Leo ligi hiyo itaendelea kwa mchezo mmoja kwenye Uwanja wa Chamazi ambapo JKT Ruvu itaonyeshana kazi na Polisi Dodoma.

Comments

  1. YANGA BOMBA-UHURU BRANCHJanuary 21, 2012 at 11:05 PM

    SAFI SANA,UMECOVER FRESH STORY YA GAME HIYO.TUKO PAMOJA.



    MDAU WA BOMBA REVERE,MASSACHUSSETTS,USA

    ReplyDelete
  2. YANGA BOMBA-UHURU BRANCHJanuary 21, 2012 at 11:10 PM

    HIVI JKT OLJORO NI TIMU YA AINA GANI WADAU,MBONA INAONEKANA KUWA TISHIO,IMEWAGONGA MTIBWA KULE KULE MASHAMBANI KWAO KULIVYO KUGUMU,KIUKWELI HII TIMU TOKA MZUNGUKO WA KWANZA NIMEKUA NIKIIFUATILIA INAFANYA VIZURI SANA,HIZI NDIO TIMU ZA KUZIPA COVERAGE KUZITIA MOYO ILI HATIMAE TUONDOKANE NA LIGI DHAIFU YA SIMBA NA YANGA TU BILA USHINDANI WA UKWELI,HONGERA SANA KWENU JKT ORJORO,MNAONYESHA NJIA KWAMBA INAWEZEKANA SIO KILA SIKU YANGA,SIMBA NA MTIBWA AU AZAM!MAMA SIMBA IFUATILIE HII TIMU TUIJUE INAVYOENDELEA

    ReplyDelete

Post a Comment