TIMU ZAPEWA SIKU SABA KUREKEBISHA USAJILI


Kwa upande wa Daraja la Kwanza, Kamati hiyo imetoa siku saba kwa klabu ambazo zimezidisha idadi ya wachezaji ili zipunguze, kwani kila timu inatakiwa kuwa na wachezaji wasiozidi 30. 
Klabu nyingi baada ya kufanya usajili wa dirisha dogo zimepitisha idadi ya wachezaji 30 wanaotakiwa kwa mujibu wa kanuni. Hivyo kwa klabu ambayo itashindwa kupunguza wachezaji ndani ya muda huo, TFF itahesabu hadi 30 na wachezaji watakaokuwa wamezidi wataondolewa. 
Kwa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL), klabu ya Villa Squad ndiyo imekutwa na kasoro katika usajili wake ambapo imetoa kwa mkopo wachezaji wanne na imepokea wengine watano kwa mkopo. 
Kwa mujibu wa kanuni ya mkopo, klabu haitakiwi kuwa na wachezaji zaidi ya watano iliotoa au kuingiza kwa mkopo kwa wakati mmoja. Hivyo Villa Squad imetakiwa kuwaandikia barua za kuwaacha wachezaji wanne iliowatoa kwa mkopo ili wawe huru (free agents).
 
Pia Kamati imeagiza viongozi wa juu wa Majeshi ambayo yanamiliki timu za mpira wa miguu kupewa elimu ya kanuni za usajili, kwani mafunzo ya kijeshi na uhamisho wa wachezaji ambao ni askari vimekuwa vikiathiri viwango vya timu zao kwenye ligi.

Comments