TASWA YAJA NA KALENDA YA 2012


MWENYEKITI WA TASWA, JUMA PINTO

KAMATI ya Utendaji ya Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) iliyokutana Novemba mwaka huu jijini Dar es Salaam ilikubaliana mambo mbalimbali ikiwemo kupanga kalenda ya matukio ya mwaka 2012 ambayo chama kinatarajia kuyafanya.
Lakini licha ya kikao kutoa mapendekezo ya matukio mbalimbali, iliiagiza Sekretarieti ya TASWA ndiyo iiweke kalenda hiyo kwenye uhalisia, kulingana na hali halisi pamoja na mfuko wa chama utakavyoruhusu. Kalenda hiyo itakapokamilika itatolewa kwa wanachama wetu na  wadau wengine.
Msisitizo mkubwa wa TASWA mwaka 2012 ni mafunzo ya aina mbalimbali kwa waandishi wa habari za michezo na wahariri wa habari za michezo kama njia mojawapo ya kuboresha taaluma ya habari.
Kutokana na hali hiyo TASWA imeandaa mafunzo ya siku tatu kuanzia Februari 20 hadi Februari 22,2012 jijini Tanga yakihusisha washiriki kutoka mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Tanga. Mafunzo yatahusu masuala ya taaluma ya habari na mambo ya michezo mbalimbali ambayo itatangazwa baadaye.
Pia Machi 19, 20 na 21 mwaka huu yatafanyika mafunzo mengine Moshi mkoani Kilimanjaro, ambayo yatahusisha wahariri wa habari za michezo na waandishi waandamizi wa habari za michezo kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Katika mafunzo hayo ya Moshi, pia zitatolewa mada mbalimbali kuhusiana na masuala ya michezo hapa nchini.

Comments