SIMBA YACHISHWA NA VICHWA NGUMU, KUWAPA KIPAUMBELE MAKINDA WAKE

PASUA kichwa inayotokana na utovu wa nidhamu wa wachezaji wake sambamba na kupunguza gharama ya fedha kwa ajili ya usajili wa wachezaji, klabu ya soka ya Simba imeamua kuelekeza nguvu zake kwa timu za vijana.

Mwenyekiti wa Simba Ismail Aden Rage alisema kwamba klabu imekuwa ikitumia fedha nyingi kwa ajili ya kusajili wachezaji toka vilabu vingine ndani nan nje ya nchini matokeo yake kushindwa kuitumikia kwa uaminifu klabu hiyo.

Alisema kuwepo kwa wachezaji wenye utovu wa nidhamu kunatokana na malezi hivyo katika kukabiliana na hali hiyo ni bora waanze kuwapandisha madaraja wachezaji wa timu zao za vijana wanazozitayarisha.

“Fikiria mtu kalelewa mtaani sijui mwingine wapi halafu anakuja Simba kufanya kazi, wapo wanaoweza kujiheshimu lakini wengine wanashindwa na matokeo yake timu inafanya vibaya kutokana na michango yao mibovu,”Alisema.

Aliongeza kuwa matunda ya kuzilea vema timu za vijana yameanza kuonekana kwa timu yao ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 kutwaa kombe la michuano ya Uhai, huku pia baadhi ya wachezaji waliopo katika kikosi cha wakubwa cha Simba wakiwa wametoka katika timu ya Vijana.

“Kwa kweli tumedhamiria kufanya mambo makubwa kupitia timu zetu za vijana ikiwemo ya miaka chini ya 17 na 20, hatutaishia kuwapandisha katika timu ya wakubwa tu, hata kuwauza katika klabu za nje,”Alisema.

Kwa sasa timu hizo za vijana zipo chini ya mkurugenzi wake Abdallah ‘King’ Kibaden huku timu ya Vijana wenye umri chini ya miaka 17 ikinolewa na Amri Said na ile ya wenye umri chini ya miaka 20 wakinolewa na Suleiman Matola.

Comments