Real Madrid inahitaji Cristiano Ronaldo kurejesha kujiamini
kwake dhidi ya Barcelona, wakati timu hizo zitakapomenyana kwenye “clasico”, mechi
ya kwanza ya Kombe la Mfalme hatua ya Robo Fainali leo.
Ronaldo amefunga mara mbili tu katika mechi 13 dhidi ya
Barcelona, bao lake la mwisho akifunga Aprili kwenye fainali ya michuano hiyo
na kuipa Madrid ushindi wa kwanza ndani ya mechi 12 dhidi ya klabu hiyo ya Catalan.
Mshambuliaji huyo wa Kireno amekuwa katika wakati mgumu
tangu apoteze nafasi kibao za kufunga mabao, siku Madrid ikipigwa 3-1 katika
mechi ya Ligi Kuu mwezi uliopita na mwaka huu amefunga bao moja tu hadi sasa.
Ronaldo ndiye anayeongoza kwa mabao yake 21 katika mbio za
kiatu cha dhahabu cha La Liga na alipagawa mno Jumamosi, wakati Madrid
iliposota kuibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Mallorca na kuiacha kwa pointi
tano Barcelona kileleni.
Wakati huo huo, mpinzani wake mkuu wa Barcelona aliyetwaa
tuzo ya tatu ya Mwanasoka Bora wa Dunia hivi karibuni, Lionel Messi, aling’ara
kwa kufunga mabao mawili akiwawezesha mabingwa hao wa Hispania kushinda 4-2 dhidi
ya Real Betis.
Mabao hayo mawili yalimfanya atimize mabao 33 msimu huu—
sita zaidi ya Ronaldo.
“Leo wakati wote amekuwa mchezaji ambaye anaweza kufanya
mabadiliko, mchezaji wa maana. Na ni mchezaji anayeendana na aina zote za
mchezo, ambaye anapenda kucheza,” alisema kiungo wa Barcelona, Xavi Hernandez.
Wakati Ronaldo anatarajiwa kuanza, kocha Jose Mourinho lazima
abadilishe mfumo wa uchezaji ambao utamuwezesha kuwasimamisha mabingwa mara 25
wa Kombe hilo, akiwakosa beki Alvaro Arbeloa na kiungo majeruhi Sami Khedira.
Mshambuliaji Angel di Maria alifanya mazoezi kwa mara ya
kwanza juzi, lakini Pepe hakufanya, ambayo inamuweka katika wakati mgumu Mourinho,
kwa sababu Mreno huyo amekuwa tegemeo la timu hivi karibuni, hususan katika
mechi za clasicos.
“Huwezi kucheza vizuri kila mechi,” alisema mshambuliaji wa Madrid,
Jose Callejon, baada ya kufunga bao la ushindi dhidi ya Mallorca.
Barcelona itamkosa mshambuliaji wake majeruhi, David Villa na
Pedro Hernandez na kiungo Seydou Keita kwenye Uwanja wa Bernabeu, ambao
mabingwa hao wa Ulaya hawajafungwa katika mechi sita.
“Tutakwenda huko ili kutafuta nafasi za kufunga mabao na
kujaribu pia kucheza soka nzuri kadiri itakavyowezekana,” alisema Pep
Guardiola.
Wapinzani hao wa jadi wa Hispania wamegawana mataji 16 ya
michuano hiyo tangu mwaka 1916 na kila timu ikishinda nane.
Mshindi wa mechi hii atacheza ama na Valencia au Levante, ambao
watamenyana kwenye Uwanja wa Mestalla kesho.
ngoma inapigwa saa ngapi hiyo
ReplyDelete