NAHODHA TWIGA APIGA MBIU

NAHODHA wa timu ya taifa ya wanawake Tanzania, Twiga Stars, Sofia Mwasikili amewaomba Watanzania hususan wanawake wajitokeze kwa wingi Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo dhidi ya Namibia kuwania kufuzu kwa fainali za Afrika kwa Wanawake (AWC) kuishangilia timu yao.
Akizungumza na Tanzania Daima jana, Mwasikili alisema kwamba timu yao iko vizuri na wamejiandaa vema kuhakikisha wanashinda mechi hiyo na kufuzu.
“Mimi ninawaomba wapenzi wa soka nchini na Watanzania kwa ujumloa waje kwa wingi Jumapili kutushangilia kutupa moyo, ili tufuzu kwani tuko vizuri na tuna morali ya ushindi,”alisema.
Twiga inahitaji hata sare katika mchezo huo ili kusonga mbele, kwani katika mchezo wa kwanza ilishinda mabao 2-0 mjini Windhoek.
Mchezo wa marudiano Jumapili hii Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kiingilio cha chini kitakuwa Sh 2,000 kwa viti vya bluu na kijani, watoto wenye umri wa chini ya miaka 10 Sh 1,000, kwa viti vya rangi ya chungwa Sh 3,000, VIP B na C Sh 5,000 na Sh 10,000 kwa VIP A. Namibia inatarajia kuwasili nchini Ijumaa (Januari 27 mwaka huu) saa 12.45 jioni kwa ndege ya South Africa Airways.

Comments