MZUNGUKO WA PILI LIGI DARAJA LA KWANZA KUANZA FEBRUARI 4


Mzunguko wa pili wa Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara inayochezwa katika makundi matatu tofauti kwa mtindo wa nyumbani na ugenini itaanza Februari 4 mwaka huu. Timu zitakazomaliza katika nafasi tatu za juu zitacheza hatua ya fainali itakayokuwa na timu tisa.
 
Kundi A lenye timu za Burkina Faso ya Morogoro, Mgambo Shooting ya Tanga, Morani ya Manyara, Polisi ya Dar es Salaam, Temeke United ya Dar es Salaam na Transit Camp ya Dar es Salaam litaanza ligi hiyo kwa mechi moja kati ya Morani na Burkina Faso itakayochezwa mkoani Manyara.
 
Februari 4 mwaka huu katika kundi B kutakuwa na mechi kati ya Small Kids ya Rukwa na Polisi ya Iringa itakayochezwa mjini Morogoro, Mbeya City na Tanzania Prisons zitaumana Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya wakati Majimaji na Mlale JKT wataoneshana kazi Uwanja wa Majimaji mjini Songea.
 
Kundi C mechi za ufunguzi zitakuwa kati ya Manyoni FC na AFC itakayofanyika mjini Singida, Rhino FC dhidi ya Polisi ya Tabora zitacheza Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora wakati 94 KJ na Polisi ya Morogoro zitakwaruzana Februari 5 mwaka huu mjini Mlandizi.

Comments