MWANDISHI WA GAZETI LA MTANZANIA AULA IDFA


MWANDISHI wa gazeti la Mtanzania, Mohamed Mharizo ameteuliwa kuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Chama cha Soka Wilaya ya Ilala (IDFA).
Uteuzi huo umefikiwa katika kikao kilichofanyika Ijumaa, Desemba 31 mwaka uliopita, chini ya Mwenyekiti wa chama hicho, Almas Kassongo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa Dar es Salaam Januari 2 na kusainiwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Daudi Kanuti, ilisema Mharizo ameteuliwa kushika wadhifa huo, kutokana na jitihada mbalimbali katika kuendeleza soka wilayani Ilala, mkoa wa Dar es Salaam na taifa kwa ujumla.
Taarifa hiyo ilisema kuwa IDFA imeridhishwa na uadilifu wa Mharizo na ukereketwa wake katika mchezo huo.

“Ni matarajio yetu ataweza kushirikiana nasi katika kuendeleza soka katika wilaya yetu na taifa kwa ujumla,” ilisema taarifa ya Kanuti.

Mharizo alipokea barua ya uteuzi huo jana kwenye Makao Makuu ya IDFA, zilizopo mtaa wa Mafia na Bonde, Kariakoo, Dar es Salaam na amesema amefurahishwa na uteuzi huo na ameahidi kufanya kazi kwa ushirikiano na viongozi wote wa IDFA kwa maslahi ya soka chama hicho na taifa kwa ujumla.
“Napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa Mwenyekiti, Katibu na Wajumbe wote wa  Kamati ya Utendaji kwa kukubali kufanya kazi nami, naamini pamoja tutafanikiwa kuendeleza soka wilayani Ilala kwa faida ya wakazi wa Ilala na taifa,” alisema Mharizo.
Mharizo pia ametumia fursa hiyo kuziomba timu zinazoshiriki Ligi ya TFF wilayani humo  na wadau wa mchezo huo kutoa ushirikiano kwa IDFA ili kufanikisha ligi hiyo iwe na msisimko zaidi.
Mharizo licha ya kuchaguliwa kuwa mjumbe wa kamati ya utendaji ya IDFA, pia ni Ofisa Habari wa timu ya Boom FC ya Ilala, mchezaji wa  timu ya soka ya Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA FC) na Mratibu wa timu ya New Habari ambao ni wachapishaji wa magazeti ya Mtanzania, Bingwa, Dimba, Rai na The African.

Comments