MATOLA AWASHANGAA WANAOMTOA SIMBA

NAHODHA wa zamani wa Simba, Suleiman Matola amezima hofu iliyoibuka kwamba ameacha kazi ya kufundisha timu B ya klabu hiyo na kwenda kufanya kazi Iringa, akisema bado yuko kazini na ana mkataba wa miaka minne.
Akizungumza na Tanzania Daima jana, Matola alisema kwamba mwezi huu wote hakuwa kazini kwa sababu alikuwa anakabiliwa na matatizo ya kifamilia na alipewa ruhusa na uongozi.
Alisema kwamba Simba ni klabu ambayo imemsaidia sana katika maisha yake kuanzia wakati anacheza hadi sasa amekuwa Kocha, yote yyakiwa matunda ya klabu hiyo.
Matola alisema kwamba kesho anamaliza likizo yake na ataanza tena kazi- na amewataka wapenzi wa Simba wapuuze uvumi wote kuhusu yeye kwamba ameacha kazi.
“Mimi ndio nimehangaika na timu hii ya vijana kuanzia kusaka wachezaji, kufundisha hadi sasa imekuwa timu imara- bingwa wa Kombe la Uhai na bingwa wa Kinesi na bado kuna matumaini makubwa mbele.
Unajua bwana, kwenye wengi pana mengi pia, nashangaa hizi habari zinatoka wapi, mimi bado kocha wa Simba B na nitaendelea na kazi kwa kuheshimu mkataba wangu,”alisema Matola.
Matola alijiunga na Simba mwaka 2000 akitokea Kagera Sugar na aliichezea timu hiyo hadi mwaka 2005 alipotimkia Afrika Kusini katika klabu ya Super Sport United ambayo aliichezea kwa misimu miwili.
Baada ya hapo, alirejea nyumbani Tanzania na kumalizia soka yake katika klabu ya Simba kabla ya kuwa kocha.     

Comments