MAN CITY YAUA 3-0

MANCHESTER, England
MANCHESTER City usiku huu walipoza machungu ya kipigo cha 1-0 kutoka kwa Sunderland, baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Liverpool kwenye Uwanja wa Etihad, Manchester na kujitanua kileleni mwa Ligi Kuu ya England.
Ushindi huo unaifanya City ifikishe pointi 48 baada ya kucheza mechi 20 na kama wapinzani wao Man United watashinda dhidi ya Newcastle leo watawafikia kwa pointi tu, ila wao wanaweza kuendelea kuongoza ligi kwa wastani mzuri wa mabao. 
Iliwachukua dakika tisa na sekunde 54 City kupata bao la kwanza, Sergio Aguero akiukwamisha mpira nyavuni kutoka nje ya eneo la penalti akiunganisha kona fupi iliyochongwa na James Milner, kufuatia shuti la Edin Dzeko kuokolewa na kipa Jose Reina.
Mwanasoka bora wa Afrika, Yaya Gnegneri Toure aliifungia City bao la pili dakika ya 32 na sekunde 31 kwa kichwa.
Bao hilo pia lilianzia kwenye kona iliyopigwa na James Milner kutoka kushoto na kumkuta Vincent Kompany aliyefumua shuti ambalo liliokolewa na Jose Reina na kuwa kona tena iliyokwenda kupigwa na David Silva kwa guu la kushoto na kumkuta Yaya aliyemaliza kazi.
James Milner alihitimisha karamu ya mabao dakika ya 74 na sekunde ya 35 kwa mkwaju mkali wa penalti, baada ya Martin Skrtel kumchezea rafu Yaya dakika ya 73 na sekunde ya 18.
Katika mchezo mwingine wa ligi hiyo, Sunderland iliendeleza wimbi la ushindi baada ya kuibwaga mabao 4-1 Wigan kwenye Uwanja wa DW. 
Mabao hayo yalitiwa kimiani na viungo Craig Gardner dakika ya nne ya nyongeza baada ya kutimu dakika 45 za kipindi cha kwanza, James McClean dakika ya 55, Stephane Sessegnon dakika ya 73 na David Vaughan dakika ya 80. Bao la Wigan lilifungwa na mshambuliaji Hugo Rodallega dakika ya 62.
Kwenye Uwanja wa White Hart Lane, bao pekee la Jermain Defoe katika dakika ya 63 lilitosha kuipa Tottenham ushindi wa 1-0 dhidi ya West Brom.
Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea tena leo kwa mchezo kati ya Newcastle dhidi ya Man Utd na Everton dhidi ya Bolton, mechi zote zikianza saa saa 5:00 usiku.
United itashuka dimbani ikiwa na kumbukumbu ya kipigo cha mabao 3-2 kutoka kwa Blackburn kwenye Uwanja wa nyumbani, Old Trafford, Jumamosi iliyiopita.
Kocha wa United, Sir Alex Ferguson, amewataka wachezaji wake kuonyesha uhai kwenye mechi ya hiyo ya ikiwa ni ya marudiano baada ya ile ya kwanza kutoka sare ya 1-1 katika Uwanja wa Old Trafford.
Mabinwga hao watetezi wa ligi hiyo walishangazwa na na kipigo hicho cha mabao 3-2, walichofungia mwaka vibaya, ingawa majirani zao City pia walipoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Sunderland, lakini Ferguson atabakia na maumivu ya kupoteza pointi hizo tatu nyumbani.
United wanajivunia rekodi yao nzuri Uwanja wa St James' Park, kwani hawajapoteza mechi tangu wachapwe mabao 4-3 mwaka 2001, ingawa watakuwa na kibarua kigumu cha kuhakikisha wanaibuka na ushindi baada ya kutoka sare ya 1-1 kwenye mchezo wa Novemba mwaka jana wakiwa nyumbani.

Comments