MALINZI AGOMBEA UENYEKITI KAGERA

KATIBU Mkuu wa zamani wa Yanga, Jamal Malinzi, atawania nafasi ya Uenyekiti wa Chama cha Soka Kagera (KRFA), ametamka bayana jana. Mdogo huyo wa Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), aliiambia DIMBA jana mchana kwamba ameamua kugombea nafasi hiyo ili kusaidia maendeleo ya soka mkoani humo. “Kwa sasa kwa kweli hali mbaya kwenye soka yetu kwa ujumla, tunahitaji kuweka mambo sawa kuanzia ngazi za wilaya, hivi mimi nimejitolea kuwania nafasi hiyo ili kuusaidia mkoa wangu huo,” alisema Malinzi. Malinzi, ambaye kwenye uchaguzi uliopita wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) alikaribia kumbwaga rais wa sasa wa shirikisho hilo, Leodegar Tenga, tayari amekwishawasiliana na uongozi wa Kagera juu ya kuwania nafasi hiyo. “Na haswa hii ilitokana na watu wa Bukoba kuniomba sana, wamekuwa wakiniomba kwa muda mrefu na sasa baada ya kutafakari ombi lao, nimeona ni wakati mwafaka kwenda kuwatumikia,” alisema Malinzi. Kwa mujibu wa barua ya Katibu wa Kamati ya Uchaguzi KRFA, Jasmeen Said, mchakato wa uchaguzi wa chama hicho unatarajiwa kuanza Januari 26, mwaka huu.

Comments